Jan 01, 2022 08:15 UTC
  • Macron: Ufaransa itakabiliwa na hali ngumu sana katika wiki kadhaa zijazo

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametahadharisha kuwa, nchi hiyo itakabiliana na hali ngumu katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo.

Katika hotuba kwa mnasaba wa mwaka mpya, Macron amesema wiki kadhaa zijazo zitakuwa za kipindi kigumu sana kwa Ufaransa kwa sababu baada ya kurekodi kesi 232,200 za watu walioambukizwa ugonjwa wa Covid-19 ndani ya muda wa saa 24 zilizopita, nchi hiyo imefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu ilipozukiwa na ugonjwa huo na kwamba ni katika mazingira hayo wanaingia kwenye shamrashara za kusherehekea mwaka mpya wa 2022.

Ripoti zinasema, kwa muda wa siku tatu mtawalia, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Ufaransa katika kipindi cha saa 24 zilizopita imepindukia laki mbili na kuifanya nchi hiyo kuwa moja ya vituo vikuu vya maambukizi ya spishi mpya ya omicron.

Katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris sherehe za jadi za michezo ya moto wakati wa usiku katika mwaka mpya zimeghairishwa, kwa sababu mamlaka husika zimesema zinachelea kufanyika kwake kukapelekea ishindikane kuwadhibiti watu. Kujumuika kwenye maeneo ya umma ya wakati wa usiku pia kumepigwa marufuku.

Katika hotuba yake hiyo kwa mnasaba wa mwaka mpya, rais wa Ufaransa amerudia tena wito wake wa kuwaomba watu wajitokeze kwa wingi kupiga chanjo akisisitiza kuwa upigaji chanjo ndio njia pekee ya kukabiliana na janga la dunia nzima la corona.../

Tags