Jan 07, 2022 07:32 UTC
  • Sisitizo la China la kuitaka Marekani iiondolee vikwazo Iran

Kabla ya kuanza duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna kuhusu JCPOA, China imeitaja Marekani kuwa mhusika katika uvurugaji mapatano ya JCPOA na hivyo imeitaka isitishe utekelezaji wa sera zake za vikwazo na mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran. Zhao Lijian Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema ni wazi kuwa, kwa mtazamo wa kisheria na kimaadili, vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mpango wa kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na Shirika la  Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA limethibitisha mara kadhaa kuwa Iran haijakengeuka mkondo wa kisheria katika shughuli zake za nyuklia. Kwa msingi huo Iran inashiriki katika mazungumzo ya Vienna kwa lengo la kutaka Marekani iiondolee vikwazo.

Wang Qun, mwakilishi mwandamizi wa China katika mazungumzo ya Vienna amesisitiza kuwa, duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna inapaswa kuendelea kwa msingi wa kujadili kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran.

Katika zama za utawala wa Donald Trump, Marekani ilikiuka mapatano ya JCPOA na hatimaye ikatangaza kujiondoa katika mapatano hayo mwezi Mei 2018 na sambamba na hilo ikatangaza kuanza vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani ambayo hutekeleza sera zake dhidi ya Iran kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni ilikuwa inadhani kuwa kwa kujiondoa katika JCPOA na kuzidisha mashikizo ya kuu kabisa, basi Iran ingesalimu amri mbele ya matakwa yake haramu. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuhusu misimamo yake ya kimsingi na si tu kuwa haijasalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani bali sasa ni Marekani ndiyo ambayo inashinikizwa na dunia irejee katika mapatano ya JCPOA na iaondoe vikwazo vya upande moja dhidi ya Iran. 

 Zhao Lijian 

Isaac Bigio, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema hivi kuhusu nukta hiyo:

"Kuhusiana na kadhia ya JCPOA, Rais Joe Biden wa Marekani anauogopa utawala wa Kizayuni wa Israel kwani makundi ya Wazayuni nchini humo yamezidisha mashinikizo dhidi yake."

Marekani sasa imezishirikisha nchi za Ulaya katika kuzidisha mashinikizo yake dhidi ya Iran na hivi sasa nchi hizo nazo zinatumia vita vya kisaikolojia ili kuishinikiza Tehran isalimu amri mbele ya matakwa haramu ya Washington.

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasimama kidete mbele ya mashinikizo ya Wamagharibi na inafanya hivyo kwa kutegemea nyaraka za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA ambalo limethibitisha kuwa shughuli zote za nyuklia za Tehran zinafanyika kwa malengo ya amani.

Iran na nchi zilizosalia katika mapatano ya JCPOA zinafahamu vyema kuwa Marekani imekiuka mapatano ya JCPOA ambayo ni makubaliano muhimu na yenye itibari kimataifa na sasa inataka kutumia mabavu kuwalazimisha wengine wafuatia mitazamo yake batili.

Barbara Slavin mtaalamu wa masuala ya kisiasa katika Baraza la Atlantiki anasema hivi kuhusu nukta hiyo:

"Njia bora zaidi ya kudhamini utekelezwaji wa mapatano ya JPOA ni pande zote kuhusika kuyatekeleza kikamilifu ili kupunguza taharuki katika maeneo yote."

Kwa vyovyote vile, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuheshimu na kufungamana na misingi yake katika JCPOA, na jambo hilo si tu limepelekea Marekani ipoteze matumaini, bali hata mashinikizo ya makundi ya Kizayuni hayawezi kuiondoa serikali ya Biden katika kinamasi ambacho Trump aliitumbukiza Marekani ndani yake.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ushiriki athirifu katika mazungumzo ya Vienna imeweza kuonyesha kivitendo kuwa inafungamana na mapatano ya kimataifa JCPOA na kwamba mpango wake wa nyuklia unafanyika kwa malengo ya amani na kamwe haitairuhusu Marekani kutekeleza sera za apathaidi au ubaguzi wa kinyuklia.

Tags