Jan 10, 2022 02:49 UTC
  • Iran yaikosoa Marekani kwa kuingiza udikteta kwenye michezo

Rais wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeikashifu na kuikosoa vikali Marekani kwa hatua yake ya kususia Michezo ya Olimpiki ya Msimu wa Baridi Kali itakayofanyika huko Beijing, China.

Reza Salehi Amiri, Rais wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki ya Iran katika barua yake kwa mwenzake wa China, Jung Wengu amesema kitendo hicho cha Marekani cha eti 'kususia kidiplomasia' mashindano hayo ya dunia kinashajiisha udikteta na ubeberu duniani.

Amesema ni jambo la kusikitisha kuiona Washington inayatumia mashindano hayo ya michezo ya dunia kama chombo cha kufikia maslahi yake ya kisiasa, kuzidisha taharuki, na kushajiisha udikteta, ubeberu na utawala wa kimabavu duniani.

Sehemu moja ya barua hiyo ya Salehi Amiri inasema kuwa: Vikwazo vya kidiplomasia dhidi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2022 ni vya kiuhasama, na njia ya wazi ya kujaribu kuyadunisha mashindano hayo.

Rais wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, hatua hiyo imeonesha sura halisi ya Marekani na waitifaki wake; na namna madola hayo ya kibeberu yanavyoweza kutumia njia zozote kushinikiza maslahi yao ghalati.

Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2022

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kiuadui na ya kiundumakuwili ya Marekani ya kujaribu kuitia ila na dosari michezo hiyo, haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuyumbisha jitihada za kutafuta umoja na mshikamano wa mataifa mbalimbali duniani kupitia michezo.

Marekani kwa kutumia kisingizio cha 'ukiukaji wa haki za binadamu', imesema wanariadha wake watashiriki kwenye michezo hiyo itakayoanza Februari 4 mwaka huu jijini Beijing, lakini haitatuma wanadiplomasia na wakurugenzi wao.

Tags