Jan 11, 2022 07:49 UTC
  • Wataalamu wa UN waitaka Marekani ifunge gereza la Guantamano

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameutaka utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani utekeleze ahadi yake ya kufunga jela ya kutisha ya Guantanamo Bay iliyoko nchini Cuba.

Mwito huo ulitolewa jana Jumatatu na wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ambao wamesisitiza kuwa, miaka 20 ya uwepo wa jela hiyo inaashiria ukurasa wenye kuchukiza na kutisha wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Taarifa ya wataalamu hao wa UN imesema: Miaka 20 ya kuwaweka kizuizini (washukiwa) kinyume cha sheria pasi na kuwapandisha kizimbani na kuwafanyia mateso na ukandamizaji, ni jambo lisilokubalika na serikali yoyote ile, hususan serikali inayodai kuwa inalinda haki za binadamu.

Wameitaka Marekani ifunge gereza hilo la kuogofya mara moja, sanjari na kuwaachia huru na kuwarejesha makwao au katika nchi ya tatu watuhumiwa wa ugaidi wanaozuiliwa kwenye jela hiyo, na iyafanye hayo kwa kuheshimu sheria za kimataifa. 

Mateso wanayoyapitia washukiwa wa ugaidi katika jela la Guantanamo

Haya yanajiri siku chache baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kutoa wito kwa Rais Joe Biden likimtaka atekeleze ahadi yake ya kufunga jela ya Guantanamo Bay.

Amnesty International ilitoa wito huo kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya miaka ishirini tangu kuanzishwa jela hiyo ya kutisha ya Guantanamo.

Tangu jela ya Guantanamo ilipoanzishwa Januari 12, 2002, takriban watu 780 wameshikiliwa katika jela hiyo na hadi sasa tuhuma za kutenda uhalifu walizobambikiwa bado hazijathibitika.

Tags