Jan 11, 2022 07:50 UTC
  • Waliohukumiwa kifo Marekani wafadhilisha 'risasi' badala ya sindano ya sumu

Wafungwa wawili waliohukumiwa kifo katika jimbo la Oklahoma nchini Marekani wameenda mahakamani kutaka kuangaliwa upya namna ya utekelezaji wa hukumu ya kifo nchini humo.

Donald Anthony Grant, ambaye aliua watu wawili katika tukio la wizi wa mabavu mwaka 2001 na Gilbert Ray Postelle, ambaye aliua watu wanne kwa kuwapiga risasi baada ya kubugia mihadarati mwaka 2005, wamemtaka Jaji Stephen Friot wa Mahakama ya Wilaya katika jimbo la Oklahoma kuchelewesha utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi yao.

Wameiomba mahakama icheleweshe hukumu dhidi yao, hadi pale mahakama itakapoamua iwapo utekelezaji wa sasa wa hukumu hiyo kwa kuchoma sindano ya sumu unaendana na katiba ya nchi hiyo au la.

Wamesema wanafadhilisha hukumu dhidi yao itekelezwe kwa njia ya kufyatuliwa risasi, badala ya njia ya sasa ya kupigwa sindano ya sumu. Wahalifu hao wamesema kuuawa kwa kufyatuliwa risasi ndio njia bora na ya haraka, na ambayo ni muhali kuandaa mazingira ya kufanyika makosa katika utekelezji wake, ikilinganishwa na njia ya sasa ya sindano ya sumu.

 

Wakili wa wawili hao waliopatikana na hatia, Jim Stronski akitetea hoja ya wateja wake amempigia mfano hai Jaji Friot akimwabia kuwa, mfungwa ambaye mwaka jana aliuawa kwa kupigwa sindano ya sumu jimboni Oklahoma, aliaga dunia zaidi ya dakika 20 baada ya kuchomwa sindano hiyo.

Amesema kabla ya mfungwa huyo kukata roho, alizirai na kupoteza fahamu zaidi ya mara 20 huku akijitapikia usoni, kabla ya kuaga dunia dakika 21 baadaye. 

Tags