Jan 11, 2022 07:52 UTC
  • Uchunguzi: Wabunge 1,700 wa Kongresi ya US wamewahi kumiliki watumwa

Uchunguzi mpya umefichua kuwa, zaidi ya watu 1,700 waliowahi kuhudumu katika Kongresi ya Marekani wamewahi kuwamiliki wanadamu kama bidhaa, hali inayoonesha biashara ya utumwa ilivyokuwa imekita mizizi nchini humo.

Uchunguzi huo uliofanywa na gazeti la Washington Post la Marekani umebainisha kuwa, kesi  1,715 za wabunge wa Kongresi ya Marekani waliowahi kuwamiliki watumwa katika maisha yao zilinakiliwa baina ya karne ya 18 na 20.

Ripoti ya uchuguzi huo iliyochapishwa jana Jumatatu inasema kuwa, wabunge wa Kongresi ya US waliokuwa wanamiliki wanadamu kama vyombo walitoka katika vyama zaidi ya 60 vya kisiasa, vikiwemo vyama mashuhuri vya Republican na Democrats.

Seneta wa chama cha Democratic, Corey Booker, ambaye ni Seneta wa nne mweusi kuchaguliwa katika Baraza la Seneti la nchi hiyo amenukuliwa na gazeti la Washington Post akisema kuwa, athari za utumwa katika jamii ya Wamarekani hazijaakisiwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Familia za Kiafrika zilivyokuwa zikitumikishwa na Wamarekani enezi za utumwa

Uchunguzi huo aidha umefichua kuwa, marais 12 kati ya 18 wa kwanza wa Marekani, wamewahi kumiliki wanadamu kama biadhaa, wakiwemo wanane ambao walikuwa na idadi kubwa ya watumwa wakiwa madarakani.

Hii ni katika hali ambayo, utumwa mambo leo unaendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali za dunia hususan katika nchi Magharibi, licha ya Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kutokomezwa utumwa duniani tangu mwaka 1951.

Tags