Jan 15, 2022 00:44 UTC
  • Mkutano usio na matunda wa Russia-NATO na kuongezeka kwa mizozo ya pande mbili

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Alexander Grushko, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Brussels mwishoni mwa mkutano wa Russia na NATO siku ya Jumatano kwamba, hitilafu za pande mbili zilikuwa wazi na kwamba katika kikao hicho kumejitokeza hitilafu nyingi.

Amesema, moja ya sababu zinazodhoofisha usalama wa Ulaya ni kuendelea kujipanua  kwa NATO kuelekea kwenye mipaka ya Russia na kwamba suala hilo halikubaliki na linatishia usalama wa nchi hiyo. Grushko ameongeza kuwa: "Tunahitaji kupata uhakikisho kwamba NATO haitajipanua zaidi kuelekea Mashariki."

Kinyume chake, maafisa wa NATO wamesisitiza misimamo yao ya hapo awali ya kupanua jumuiya hiyo upande wa Mashariki na kupeleka wanajeshi kwenye mipaka ya Russia. Akijibu msimamo wa Russia, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema kuwa muungano huo wa kijeshi hautaacha sera yake ya milango wazi na haki yake ya kupeleka majeshi karibu na Russia. Katibu Mkuu wa NATO ameongeza kuwa: "Hatutalegeza kamba kuhusu haki ya mamlaka ya nchi yoyote ya Ulaya au ardhi ya nchi hiyo."

Maana ya Stoltenberg kuhusu siasa za milango wazi za NATO ni sera za shirika hilo za kujitanua zaidi upande wa Mashariki na kuzipa uanachama katika jumuiya hiyo ya kijeshi ya Magharibi nchi za kandokando ya Russia kama Ukraine na Georgia.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg

Kwa upande mwingine, NATO imepeleka wanajeshi na zana za kivita huko Ulaya Mashariki, haswa nchi jirani na Ukraine na Russia kwa kisingizio cha uwezekano wa shambulizi la kijeshi la Russia dhidi ya Ukraine,  na vilevile katika Bahari ya Baltic na Bahari Nyeusi; kitendo ambacho kimsingi kina maana ya mzingiro wa kijeshi na kuidhibiti Russia.

Ujumbe wa Russia ulipaswa kukutana na wawakilishi wa NATO kujadili mapendekezo ya Rais Vladimir Putin kuhusu udharura wa kupewa dhamana za kisheria kwamba Magharibi itaachana na fikra zake za kupanua shirika na NATO kuelekea Mashariki, kujiunga Ukraine na NATO na kuanzishwa kambi za kijeshi katika jamhuri za Soviet ya zamani. NATO kwa upande wake imekataa pendekezo hilo. Robyn Dixon, mwandishi wa habari wa Marekani na mtaalamu wa siasa anasema: "Katika mkutano huo wa karibu masaa manne, wanachama wote 30 wa NATO waliunga mkono sera ya "milango wazi " ya shirika hilo la kijeshi, na kwamba zitazikubali  Ukraine au Georgia kama nchi wanachama baada ya kukamilisha masharti ya kujiunga."

Kwa hivyo, kama ilivyotarajiwa, mazungumzo ya pande mbili za Russia na NATO katika mkutano wa Jumatano huko Brussels hayakuwa na matokeo chanya, na pande zote mbili ziling'ang'ania misimamo yao ya hapo awali. Jambo muhimu hata hivyo ni kuwa, Moscow ilitangaza baada ya mkutano huo kwamba, itazingatia hatua zote za kukabiliana na ongezeko la vitisho vya usalama vinavyoletwa na NATO. Kuhusiana na suala hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Alexander Grushko amesema kuwa, upinzani wa NATO dhidi ya mapendekezo ya Moscow unaweza kusababisha mvutano na migogoro zaidi na kuongeza kuwa: "Iwapo hatuwezi kufikia makubaliano na NATO, tuko tayari kwa chaguo lolote."

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Alexander Grushko

Inatazamiwa kuwa, mivutano ya pande mbili kati ya Moscow na nchi za Magharibi itaongezeka na kupanuka zaidi baada ya kushindwa mazungumzo ya usalama kati ya Russia na Marekani mjini Geneva na kufeli mkutano wa kilele wa Russia na NATO.

Tags