Jan 15, 2022 00:46 UTC
  • Taliban yaitaka US iheshimu wito wa UN wa kuachia fedha za Afghanistan

Serikali ya Taliban imeitaka Washington itekeleze mwito uliotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa, wa kuachia fedha za Afghanistan zilizozuiwa nchini Marekani.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid alitoa mwito huo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter hapo jana na kueleza kuwa: Marekani inapaswa kutoa jibu chanya kwa mwito wa jamii ya kimataifa, na kuachia fedha za Afghanistan.

Siku ya Alkhamisi, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliitaka Marekani ichukue hatua ya kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu nchini Afghanistan. Marekani inashikilia karibu dola bilioni 9.5 za Benki Kuu ya Afghanistan.

Mwito wa Taliban umekuja siku chache baada ya Umoja wa Mataifa na washirika wake kuzindua mpango wa kusaidia watu milioni 28 wenye uhitaji mkubwa wa misaada ya kubinadamu nchini Afghanistan. Mpango huo uliozinduliwa Jumatatu iliyopita mjini Geneva Uswisi unahitaji dola bilioni 4.44, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi cha msaada wa kibinadamu kuwahi kuzinduliwa.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid

Kundi la Taliban lilitwaa madaraka nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka uliopita, sambamba na kuondoka askari wa Marekani katika nchi hiyo baada ya vita vya miaka 20.

Umoja wa Mataifa umewahi kutoa indhari mara kadhaa ukieleza kwamba, kama hali ya sasa ya Afghanistan haitashughulikiwa kwa wakati, basi asilimia 97 ya wananchi wa nchi hiyo watakuwa chini ya mstari wa umasikini hadi kufikia katikati mwa mwaka huu 2022.

Tags