Jan 16, 2022 02:43 UTC
  • Kukosolewa vikali rekodi ya haki za binadamu ya serikali ya Biden

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa rekodi ya haki za binadamu ya serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani na kuitaja kuwa inatia wasiwasi. Human Rights Watch imebainisha hayo katika ripoti yake ya hali ya haki za binadamu duniani katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa mwaka mpya wa 2021.

Ripoti iliyowekwa katika tovuti ya shirika hilo la haki za binadamu imesisitiza kuwa, serikali ya Biden imepiga hatua chache katika suala la usawa wa watu wa mbari tofauti na wa kijinsia nchini Marekani licha ya matamko yake kuhusu kuwajibika katika uwanja huo. 

Licha ya serikali ya Biden kutao madai mengi ya kutetea haki za binadamu na kuunga mkono suala hilo, inatupasa kuona kwamba je, Washington ipo tayari kutambua ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoshuhudiwa ndani ya Marekani kwenyewe na kuchukua hatua za kukomesha suala hilo au la? Jibu la swali hili ni hapana. Hii ni kwa sababu licha ya madai hayo lakini serikali ya Biden haijachukua hatua yoyote kwa ajili ya kukomesha ubaguzi wa kimbari na wa kijamii nchini Marekani. 

Nicole Austin-Hillery, Mkurugenzi wa HRW nchini Marekani 

Nicole Austin-Hillery Mkurugenzi wa shirika la HRW nchini Marekani anasema: Raia weusi nchini Marekani wangali wanateseka na dhulma kubwa za kiuchumi zinazosababishwa na ubaguzi wa rangi wa kimfumo uliopo nchini humo ambao umeathiri vizazi mbalimbali huku sera za mipaka za nchi hiyo zikifutilia mbali haki ya wahajiri kupewa hifadhi. Vilevile maafisa wa mipakani wa Marekani wamekuwa wakiamiliana kwa mabavu na kuwadhalilisha wahajiri.

Mashirika ya haki za binadamu kama vile Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa yameripoti ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na ubaguzi mkubwa na uliokita mizizi wa rangi, ukiukwaji wa haki za wafungwa, ukiukwaji wa haki za wenyeji wa Amerika, ukiukwaji wa haki za wanawake, unyanyasaji na ukatili unaofanywa dhidi ya wahamiaji haramu na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na kadhalika. Ukosoaji mkubwa zaidi wa  Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ulijikita katika hali mbaya inayowakabili raia weusi nchini Marekani pamoja na ubaguzi wa rangi wa kimfumo unaofanyika nchini humo, na kutoa wito wa kufanyika mabadiliko katika uwanja huo. Pamoja na hayo, serikali ya Marekani imekuwa ikipuuza miito ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.   

Ni dhahir shahir kuwa, miongoni mwa ukiukaji wa waziwazi wa haki za binadamu huko Marekani, nchi ambayo  kwa mamia ya miaka sasa inadai kuwa mbeba bendera na mtetezi wa haki na uhuru wa binadamu, ni vitendo vya kibaguzi na ukatili wanavyofanyiwa raia weusi.  Ripoti ya Shirika la Human Rights Watch imesisitiza kuwa, kuwafunga jela raia weusi huko Marekani na ubaguzi wa rangi wa kimfumo ambavyo ni miongoni mwa vielelezo vya ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, vingali vinatekelezwa nchini humo. Takwimu za mauaji yanayofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya raia weusi ni mara tatu ya zile zinazohusiana na wazungu wa nchi hiyo; na licha ya kwamba raia weusi wenye asili ya Afrika wanaunda asilimia 12.4 ya jamii ya Marekani, lakini asilimia 24 ya watu wanaonyongwa nchini humo ni raia weusi. 

Marekani

Ni wazi kuwa, ubaguzi wa rangi na ubaguzi katika masuala ya kupata elimu na ajira, ukandamizaji, ukatili na uonevu dhidi ya raia weusi wa Marekani vimekuwa mambo ya kawaida kabisa nchini humo. 

Katika miaka ya karibuni kufuatia kuongezeka sana idadi ya Walatino katika jamii ya Marekani, jamii hiyo pia imeathiriwa na vitendo vya ubaguzi wa kimbari na utumiaji mabavu. Jamii za walio wachache ndizo zilizoathirika na kudhurika pakubwa huko Marekani kufuatia kuenea maambukizi ya corona. Kuhusu suala hilo, ripoti ya HRW inaonyesha kuwa, jamii ya raia weusi, Walatino na raia asilia wa Marekani wameathirika kwa kiasi kikubwa na COVID-19; na suala hilo limezidisha ukosefu wa usawa baina ya raia nchini Marekani katika maeneo ya huduma za afya, makazi, upatikanaji wa maji salama, ajira, elimu, na kuzidisha ulimbikizaji wa utajiri na mali kwa makundi mengine. Ukosefu wa usawa wa kiuchumi pia bado unaendelea kupanuka katika nchi hiyo kubwa zaidi ya kibepari duniani hususan baina ya raia weusi na wazungu.

Bernie Sanders

Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa Marekani ambaye anakosoa vikali ufa na hitilafu kubwa za kimatabaka zinazoshuhudiwa katika jamii ya Marekani anasema: "Hii leo matajiri wakubwa wanazidi kutajirika, huku mamilioni ya familia za tabaka la wafanyakazi wakihangaika kupata riziki au kulipa bili zao. Tuko katika hali mbaya ambapo pengo kati ya matajiri na maskini nchini Marekani ni kubwa kuliko kipindi chochote katika miaka 100 iliyopita."

Tags