Jan 16, 2022 12:06 UTC
  • Waziri Mkuu wa Uingereza ashinikizwa ajiuzulu kutokana na kashfa ya corona

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson yuko chini ya mashinikizo ya kujiuzulu kutokana na kashfa inayomkumbwa ya kushiriki katika mjumuiko wa sherehe za watu wengi kinyume cha sheria za kudhibiti maambukizi ya COVID-19.

Gazeti la Habari la Independent limeandika kuwa Johnson sasa anataka kuwafuta kazi baadhi ya mawaziri ili kunusuru nafasi yake kufuatia kashfa hiyo inayojulikana kama Partygate.

Johnson na wenzake kadha wanatuhumiwa kufanya dhifa ya zaidi ya watu 100 kwenye makaazi rasmi ya kiongozi huyo mnamo Mei 2020 wakati ambao sherehe kama hizo zilikuwa zimezuiwa kisheria. 

Ufichuzi huo ambao yumkini utakuwa na taathira kubwa kwa kiongozi huyo, unafuatia madai mengine kama hayo yaliyotolewa mwezi uliopita kwamba ofisi yake ilifanya sherehe kadhaa kuelekea sikukuu ya krismasi mwaka 2020, licha ya kwamba mikusanyo ilikuwa imepigwa marufuku.

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeandika kuwa wananchi wamepoteza imani na Boris Johnson  na chama chake cha Conservative huku chama cha upinzani cha Leba kikiendelea kupata umashuhuri.

Bunge la Uingereza

Swali sasa ni lini na vipi Johnson atafukuzwa kazi, kwa kura ya kutokuwa na imani naye - kwa mfano - ambayo itafanya kujiuzulu kwake kuwa moja kwa moja.

Hata kutoka kwenye chama chake, baadhi ya wabunge wanamtaka aondoke serikalini. Kwa hivyo Boris Johnson anaweza kulazimishwa kujiuzulu, shinikizo kutoka kwa chama chake na kutoka kwa serikali ikiwa kura za kutosha zitakusanywa kati ya walio wengi.

Kuna majina ya wanasiasa kadhaa ambao wanatajwa kuwa wenye uwezo wa kuchukua nafasi ya Johnson na miongoni mwao ni Waziri wa Fedha Rishi Sunak, Waziri wa Mambo ya Nje Liz Truss na Dominic Raab, Waziri wa Sheria wa sasa ambaye alichukuwa nafasi ya Boris Johnson alipoambukizwa virusi vya Corona.