Jan 16, 2022 12:18 UTC
  • Animesheni yapelekea Twitter ifunge akaunti inayofungamana na Kiongozi Muadhamu

Mtandao wa kijamii wa Marekani, Twitter, umetangaza kufunga ukurasa wa Twitter unaofungamana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Sayyed Ali Khamenei kutokana na kuchapishwa klipu ya animesheni inayohusu kuuawa shahidi kamanda shujaa wa Iran katika vita dhidi ya ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Msemaji wa Twitter aliliambia shirika la habari la AFP Jumamosi kuwa, akaunti ya @KhameneiSite 'imesimamishwa kwa muda' kutokana na kile ambacho kimetajwa ni ukiukaji wa sera za mtandao huo wa kijamii.

Hali hiyo imekuja baada ya akaunti hiyo ya Twitter kuweka klipu kuhusu ahadi ya Iran ya kulipiza kisasi damu ya Kamanda Soleimani ambaye aliuawa kigaidi Januari 2020 kufuatia amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump.

Hii si mara ya kwanza kwa mashirika ya mitandao ya kijamii ya Marekani kujaribu kuzuia maelezo yanayohusiana na kamanda huyo Muirani ambaye aliongoza vita dhidi ya ugaidi.

Hivi karibuni wakati wa kukumbuka mwaka wa pili tokea auawe shahidi Kamanda Solemani, mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook iliondoa chochote kile klichoonekana kumuunga mkono Kamanda Soleimani katika hatua iliyotajwa kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa maoni na kujieleza.

Shahidi Qassem Soleimani

Ikumbukwe kuwa, Tarehe 3 Januari 2020 serikali ya Marekani ilimuua kigaidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mji mkuu wa Iraq pamoja na baadhi ya wasaidizi wake, akiwemo Abu Mahdi al-Mohandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi wa Iraq ya al Hashdu al Shaabi. Mauaji hayo ya kinyama yalifanyika kwa agizo la Donald Trump Rais wa wakati huo wa Marekani.

Kufuatia mauaji hayo ya kigaidi, tarehe 8 Januari yaani siku tano baada ya tukio hilo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilivurumisha makombora kadhaa ya balestiki na kuilenga kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ainul-Asad katika mkoa wa al-Anbar nchini Iraq. Baada ya tukio hilo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilitangaza hatua kwa hatua kwamba, askari wake 110 waliokuwa katika kambi hiyo walijeruhiwa na kupata madhara ya ubongo na hivyo kuwa chini ya uangalizi wa kitiba.