Jan 17, 2022 04:40 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mapatano ya Iran na China ni ushindi kwa mataifa mawili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema mapatano ya miaka 25 ya kistratijia baina ya Iran na China ni ushindi kwa mataifa yote mawili kwani yanakidhi maslahi ya pande mbili.

Akizungumza na Televisheni ya Kimataifa ya China (CGTN), Amir-Abdollahian amesema: "Mapatano haya yamejumuisha kila kitu kwa maslahi ya nchi mbili." Ameongeza kuwa, Tehran na Beijing zitanufaika na mkataba huo ambao ulianza kutekelezwa Ijumaa.

Mapatano hayo yanalenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kiuchumi na kisiasa baina ya Iran na China na yanatazamwa kama tukio la kihistoria katika uhusiano wa pande mbili.

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitembelea China kufuatia mwaliko wa waziri mwenzake wa China Wang Yi.

Amir-Abdollahian ameiambia CGTN kuwa, katika mazungumzo yake na maafisa wa China, wamejadili njia za kutekeleza mapatano hayo na pia masuala muhimu ya kimataifa pamoja na mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na pande tano zilizo katika mapatano ya JCPOA, China ikiwemo.

Amesema mjumbe wa China katika mazungumzo ya Vienna amekuwa na nafasi muhimu katika kuunga mkono haki za kinyuklia za Iran ambapo amekuwa akisisitiza haja ya kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.