Jan 18, 2022 13:25 UTC
  • Wimbi la wakimbizi wanaoelekea barani Ulaya laongezeka sana

Umoja wa Ulaya umesema kuwa, wimbi la wakimbizi wanaongia barani humo limeongezeka sana hivi sasa baada ya kupita kipindi kifupi cha kuzorota kidogo wimbi hilo.

Gazeti la kila siku la El País la nchini Uhispania limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, takwimu za karibuni kabisa zilizotolewa na shirika la kulinda mipaka ya Umoja wa Ulaya zinaonesha kuwa, mwaka 2021, wakimibizi laki moja na 90,000 waliingia barani Ulaya idadi ambayo inakaribia rekodi ya mwaka 2017 ambapo karibu wakimbizi laki mbili na 4 waliingia kwenye nchi za bara hilo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, suala la kuongezeka wimbi la wakimbizi wanaomiminika barani Ulaya linatokana na kuongezeka ukosefu wa usawa na uadilifu duniani baada ya kuenea janga la ugonjwa wa UVIKO-19, kuzuka mapigano mapya na hata ongezeko la joto duniani. 

Gazeti la El Pais la Uhispania

 

Nalo  Shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu la Oxfam limetangaza kuwa, licha ya watu katika maeneo mbalimbali ya dunia kuwa maskini zaidi katika kipindi cha tangu kuibuka maradhi ya corona, lakini dhulma na ukosefu wa usawa nao umeongezeka.

Ripoti ya Oxfam imeeleza kwamba, katika kipindi cha kuzuka ugonjwa wa UVIKO-19 au corona, mbali na kuongezeka umasikini duniani, lakini pia utajirii wa matajiri kumi duniani umeongezeka maradufu.

Pia shirika hilo la Oxfam limesema, kipato cha asilimia 99 wa wakazi wa dunia kimekuwa kibaya mno katika kipindi hiki cha janga la corona lakini kundi la mamilionea ulimwenguni, utajirii wao umeongezeka kwa takribani dola trilioni tano kiwango ambacho kinahesabiwa kuwa ongezeko kubwa zaidi katika kipato chao.