Jan 19, 2022 02:40 UTC
  • Kukua uchumi wa Venezuela licha ya miaka kadhaa ya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani

Licha ya njama mtawalia za Marekani za kuhakikisha Venezuela inatengwa kieneo na kimataifa, lakini Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini ametangaza kuwa, Venezuela imerejea katika mkondo wa ustawi na kukua uchumi wake licha ya miaka kadhaa ya njama hizo za Marekani.

Rais Maduro sambamba na kuashiria kwamba, baada ya miaka minne ya ughali na kupanda gharama za maisha kulikotona na vikwazo vya Marekani, katika mwaka uliomalizika hivi karibuni wa 2021, mwenendo wa kukua uchumi nchini humo umerejea na uzalishaji mafuta umekaribia mapipa milioni moja kwa siku amesisitiza kuwa, serikali ya Caracas inaendelea na juhudi zake kuhakikisha kuwa, inafikia uzalishaji wa mapipa milioni mbili ya mafuta kwa siku.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Marekani imefanya njama nyingi na za kila upande kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Venezuela inayoongozwa na Rais Nicolas Maduro. Katika uwanja huo, utawala wa Marekani ukiwa na nia ya kutimiza malengo yake hayo haramu imetekeleza njama tofauti kama mashinikizo ya kiuchumi na vikwazo mbalimbali katika uga wa kisiasa na kiuchumi dhidi ya Venezuela. Miongoni mwa njama muhimu vya Marekani katika uwanja huo ni kuliwekea vikwazo Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela.

Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, serikali ya Marekani imepiga marufuku kununuliwa nishati ya mafuta kutoka kwa Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela kama ambavyo ikiwa mataifa mengine au mashirika ya kigeni yatatumia mfumo wa fedha wa Marekani katika biashara yao ya mafuta na Venezuela, basi yatajumuishwa pia katika vikwazo hivyo vya Washington.

Kushadidisha vikwazo, kufanya njama za mapinduzi, kuwaimarisha wapinzani wa ndani nchini Venezuela na kuwapatia bajeti na suhula wapinzani wa Venezuela ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Washington dhidi ya serikali ya Rais Maduro.

Njama hizo za Marekani zilifikia kilele pale serikali ya Washington ilipotangaza kumuunga mkono kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido na mwaka 2019 kumtambua kinara huyo wa upinzani kama Rais wa Venezuela. Pamoja na hayo, hatua na njama zote za Marekani za kutaka kuiangusha serikali halali ya Venezuela zimeshindwa na kugonga ukuta.

Venezuela ambayo kipindi fulani ilikuwa nchi tajiri zaidi katika eneo la Kusini mwa Amerika ya Latini, katika miaka ya hivi karibuni licha ya kuwa na akiba kubwa kabisa ya mafuta duniani, mwaka 2019 iliporomoka na kuwa katika nafasi ya 21 ya nchi inayozalisha mafuta na kusafirisha mafuta kutoka nafasi ya 12 iliyokuwa ikishikilia mwaka 2017. Takwimu zinaonyesha kuwa, katika mwaka 2020 uzaliashaji mafuta wa Shirika la Taifa la Mafuta la Venezuela ulifikia mapipa 376,500 kwa siku.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchin Venezuela anayeungwa mkono na kusaidiwa na Marekani

Chuo cha Mision Verdad hivi karibuni kiliandika katika ripoti yake: Mzingiro wa kiuchumi, vikwazo, kuzuia mali na fedha za Venezuela na kuzuia nchi hiyo kufanya mazungumzo katika soko la kimataifa ni mifano tu ya hatua za Marekani za kuiwekea vikwazo Venezuela ikiwa na lengo la kufikia malengo yake.

Kimsingi ni kuwa, licha ya kuweko mibinyo na mashinikizo hayo, lakini viongozi wa Venezuela wametekeleza sera mpya na kupanua mahusiano ya kisiasa na kiuchumi na mataifa mengine ya dunia kama Russia, China na Iran ili kuondoa mapungufu ya nchi yao na hivyo kuleta ahueni katika masuala mbalimbali ikiwemo kadhia ya uchumi.

Hatua zilizochukuliwa na Venezuela  zimeifanya nchi hiyo licha ya mashinikizo hususan baada ya kuibuka maradhi ya Covid-19 ambayo yamebana uga wa ushirikiano wa matiafa na kuwa na taathira hasi kwa uchumi wa dunia, kuweza  kuhuisha usafirishaji nje ya nchi mafuta ghafi na kuweza kwa namna fulani kudhibiti upandaji wa gharama za maisha.

Fernando Ferreira, mweledi na mtaalamu wa kituo cha ushauri wa nishati cha Rapidan anasema kuhusiana na hilo kwamba: Mwenendo wa uzalishaji mafuta wa Venezuela umekuwa chanya na uwezekano wa kuzalisha mapipa milioni moja kila siku ni jambo linalowezekana.

Kwa kuzingatia mafanikio haya Rais Maduro ametoa ahadi kwamba, mwaka huu utashuhudia kuhuika uchumi wa nchi hiyo na chimbuko la hilo ni juhudi mtawalia za uchumi unaotegemea uzalishaji wa ndani.

Inaonekana kuwa, filihali Venezuela na mataifa mengine yaliyo chini ya mashinikizo ya Marekani katika eneo la Amerika ya Latini, yataweza kuvuka kipindi hiki na kufanikiwa kutatua matatizo yanayowakabili kupitia umoja na kuimraisha ushirikiano wao wa kieneo na kimataifa, hatua ambayo itakuwa pigo kubwa dhidi ya Marekani pamoja na washirika wake.

Tags