Jan 19, 2022 10:19 UTC
  • Mgombea wa kiti cha urais Ufaransa asisitiza kujitoa Paris ndani ya Nato

Mgombea wa kiti cha urais nchini Ufaransa wa mrengo wa kushoto wa Kisoshalisti ameashiria ulazima wa Ufaransa kujitoa katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) na kusisitiza kuwa kuna udharira kwa Paris na Moscow kufanya mazungumzo ili kujiepusha na mivutano.

Jean-Luc Mélenchon amekariri tena msimamo wake dhidi ya Nato na kusisitiza juu ya ulazima wa Paris kujitoa katika Muungano wa Nato na kusema: Ni jambo la dharura kwa Ufaransa kuwa huru katika masuala ya kijeshi. 

Mwanasiasa huyo mgombea wa kiti cha urais nchini Ufaransa aidha ameashiria namna jumuiya ya Nato ilivyoasisiwa kwa lengo linalofahamika la kukabiliana na Umoja wa Kisovieti na kwamba Ufaransa kuwa mwanachama ndani ya Nato ni kinyume na msingi wa kujitawala na mamlaka ya umoja wa nchi hiyo. 

Mwanasiasa huyo wa mrengo cha kushoto wa Ufaransa ameongeza kuwa, Ufaransa inapasa kuwa huru na kutoitegemea Marekani katika masuala ya silaha kutokana nguvu ya nyuklia iliyonayo.  

Mélenchon wakati huo huo ameunga mkono mazungumzo kati ya Ufaransa na Russia na kueleza kuwa kisiwa cha Crimea ni mali ya Russia. Aidha amezitaja kuwa hatari sera dhidi ya Russia zinazotekelezwa na serikali ya sasa ya Ufaransa na kulaani pia kushadidishwa hali ya mvutano dhidi ya Moscow kusiko na msingi wowote. 

Kisiwa cha Crimea 

Uhusiano wa Russia na Marekani pamoja na Nato umekuwa katika hali ya mivutano na misuguano katika miezi ya karibuni huku Moscow ikionya kuwa itatoa jibu la kijeshi iwapo silaha na zana za kijeshi za Nato zitapelekwa karibu na mipaka ya Russia.