Jan 20, 2022 04:30 UTC
  • Covid-19 imeandaa mazingira ya kushadidi ukosefu wa usawa na uadilifu duniani

Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu la Oxfam limetangaza kuwa, mbali na watu katika maeneo mbalimbali ya dunia kuwa maskini zaidi katika kipindi cha tangu kuibuka maradhi ya corona, dhulma na ukosefu wa usawa nao umechukua mkondo wa kuongezeka.

Ripoti ya Oxfam imeeleza kwamba, katika kipindi cha kuibuka na kusambaa maradhi ya Covid-19 mbali na umasikini kuongezeka, utajiri wa matajiri kumi duniani umeongezeka maradufu.

Taarifa ya shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu la Oxfam imeeleza pia kuwa, hali ya kipato cha asilimia 99 wa wakazi wa dunia imekuwa mbaya mno katika kipindi hiki cha maradhi ya Covid-19.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya OXFAM, imeashiria jinsi dhulma na ukosefu wa usawa ulivyoongezeka katika kipindi cha mlipuko wa corona na kueleza katika ripoti yenye anuania isemayo "Ukosefu wa Usawa Unaoua" kwamba: Kundi la mamilionea ulimwenguni, utajirii wao umeongezeka kwa takribani dola trilioni tano kiwango ambacho kinahesabiwa kuwa ongezeko kubwa zaidi. Sambamba na kuongezeka utajri wa matajiri, asilimia 99 ya wakazi wa dunia wamezidi kuwa masikini huku watu milioni 160 duniani wakiishi katika umasikini wa kupindukia, imeeleza ripoti hiyo ya shirika la OXFAM.

 

India ni miongoni mwa nchi ziliazoathiriwa vibaya na Corona na hivyo kuvuruga uchumi na kuongezeka idadi ya masikini

 

Katika akthari ya maeneo ya dunia hususan katika nchi nyingi za Kiafrika na baadhi ya mataifa ya Amerika ya Latini, kunashuhudiwa ukosefu wa usawa na uadilifu katika sekta ya tiba, afya sambamba na kukosekana uwezekano wa kuzifikia huduma za afya, suuhula za kitiba, dawa na hata uhaba wa chanjo. Mwenendo huu umepelekea kupotea bure bilashi roho za watu wengi duniani.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, takribani asilimiai 67 ya watu katika mataifa ambayo yana kipato cha juu, kwa akali wamepokea dozi moja tu ya chanjo ya Corona. Hii ni katika hali ambayo, watu chini ya asilimia 10 katika mataifa yenye kipato cha chini hadi sasa hawajafanikiwa kupata hata dozi ya kwanza ya Covid-19.

Ukosefu huu wa usawa na uadilifu ambao umetajwa na Shirika la Afya Dunani (WHO) kuwa ni kashfa ya kimaadili unaweza kuwa mkubwa zaidi ya ilivyo hivi sasa kwani mataifa mengi yanafanya juhudi za kujilimbikizia dozi za ziada za chanjo kufuatia kuibuka spishi mpya ya kirusi cha Corona cha Omicron.

Uhaba wa bidhaa za chakula, kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira ni jambo jingine linashuhudiwa hasa katika mataifa dhaifu. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa, watu wasiopungua milioni 155 wamo katika kipindi kigumu mno cha mgogoro wa usalama wa chakula, idadi ya ambayo ni ongezeko la watu milioni 20 ikilinganishwa na mwaka jana (2021).

Moja ya mambo yanayolalamikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni ukosefu wa uadilifu katika ugavi wa chanjo ya Covid-19 huku mataifa tajiri yakijilimbikizia chango za ziada

 

Kuendelea vita na mapigano katika akthari ya mataifa ya dunia na kudhamini gharama za kijeshi ni mambo mengine ambayo kwa hakika yameshadidisha ukosefu wa usawa. Ghama za kijeshi katika mataifa ya dunia licha ya kuibuka maradhi ya Covid-19 zimeongezeka mpaka kwa asilimia 15. Gharama hizo ni mara sita ya hitajio la bajeti ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupambana na baa la njaa.

Abby Maxman, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu la Oxfam anasema: Hii leo matokeo mabaya yaliyosababishwa na taaathira hasi kwa uchumi kufuatia kuibuka na kusambaa virusi vya Corona yamekuwa makubwa zaidi. Mataifa yaliyoko vitani badala ya kupambana na msambao wa virus vya Corona yameendelea kuelekeza nguvu zao vitani ambapo aghalabu itakuwa ni pigo kwa mamilioni ya watu duniani ambao hapo kabla tayari walikuwa wamedhurika kutokana na majanga ya hali ya hewa na kutetereka uchumi.

Hata kama ukosefu wa usawa na uadilifu ulikuweko duniani hata kabla ya kuibuka virusi vya Corona, lakini inaonekana kuwa, maradhi ya UVIKO-19 yameongeza kasi ya dhulma hiyo kiasi kwamba, pengo la tabaka la juu na la chini katika jamii limezidi kuongezeka.

Hivi karibuni Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeashiria kushadidi ukosefu wa usawa na uadilifu na kutangaza kuwa, viwango vya haki za binadamu katika mfungamano na malengo ya ustawi wa kudumu vinapaswa kupewa kipaumbele katika hatua na juhudi zinazofanyika kwa ajili ya kuikwamua dunia na msambao wa corona. Hata hivyo inaonekana kuwa, maonyo na indhari hizi kwa mataifa makubwa na matajiri wa dunia ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Tags