Jan 20, 2022 08:13 UTC
  • Maseneta wa Ufaransa wapasisha mpango wa kupiga marufuku hijabu michezoni

Baraza la Seneti la Ufaransa limepiga kura na kupasisha sheria inayopiga marufuku uvaaji wa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo.

Hatua hiyo ambayo ni muendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu inatarajiwa kuzusha makelele na malalamiko mengi wakati mji mkuu wa Ufaransa Paris unatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki mwaka 2024.

Maseneta 160 walipiga kura ya ndio kuunga mkono marufuku hiyo huku wenzao 143 wakipinga.

Hata hivyo haijafahamika kama marufuku hiyo itajumuisha mashindano ya michezo ya Olimpiki hapo mwaka 2024 au la.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, endapo marufuku hiyo itajumuisha mashindano ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Parsi mwaka 2024 huenda mashindano hayo yakakabiliwa na changamoto kubwa.

Hii ni kutokana na kuwa, kama wanamichezo Waislamu watasusia mashindano hayo itakuwa pigo kubwa hasa kwa kuzingatia kuwa, katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020 wanamichezo Waislamu walikuwa na nafasi na hisa kubwa ya medali katika mashindano hayo.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

 

Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ufaransa huko nyuma limewahi kuchukua hatua za chuki dhidi ya Uislamu ambapo lilikuwa likiwakataza wanawake Waislamu kuvaa kitambaa cha kichwa katika mashindano rasmi ya michezo.

Huko nyuma pia Baraza la Seneti la Ufaransa limewahi kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.

Tangu Rais Emmanuel Macron aliposhika hatamu za uongozi nchini Ufaransa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kuvunjiwa heshima matukufu ya  Uislamu vimeongezeka mno katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Tags