Jan 20, 2022 10:04 UTC
  • Viongozi wa Russia wasisitiza kuimarisha uhusiano na Iran

Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Russia, Duma, amesena katika mazungumzo yake na Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa uhusiano wa nchi mbili hizi ni mzuri na kuongeza kuwa kuimarishwa uhusiano huo hadi kiwango cha ushirikiano wa kistratijia ni suala muhimu sana kwa Russia.

Amir Abdollahian ambaye yuko kwenye safari ya ujumbe unaoongozwa na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu mjini Moscow Russia, jana Jumatano alionana na kuzungumza na Leonid Slotsky, Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Russia ambapo walizungumza na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yenye umuhimu kwa nchi mbili.

Walijadiliana kwa kina kuhusu uhusiano wa nchi mbili na mabunge ya nchi hizi na kusisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano huo katika nyanja zote.

Leonid Slotsky

Amir Abdollahian ameashiria mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya marais wa nchi hizi ambao wamejadili masuala muhimu yanayohusu nchi zao na kusema kuwa mazungumzo hayo bila shaka yataziweka nchi hizi katika njia inayofaa ya kistratijia.

Leonid Slotsky pia amesema uhusiano wa mabunge ya nchi mbili ni mzuri na unaoridhisha na kuongeza kuwa ushirikiano wa kistratijia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una umuhimu mkubwa kwa Russia.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran aliwasili mjini Moscow hapo jana Jumatano akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni katika kujibu mwaliko aliopewa na rais mwenzake wa Russia Vladimir Putin.

Tags