Jan 20, 2022 12:08 UTC
  • Vijidudu-maradhi sugu vyaua watu wengi zaidi kuliko saratani, UKIMWI na malaria

Utafiti mpya uliofanywa na jarida la kitiba na kisayansi la The Lancet unaonyesha kuwa vijidudu-maradhi vikubwa na sugu sasa vinaua watu wengi zaidi kuliko saratani, UKIMWI na malaria.

Kulingana na uchunguzi wa jarida la kitiba la The Lancet, zaidi ya watu milioni 1.2 ulimwenguni  hupoteza maisha kila mwaka kutokana na maambukizi ya kawaida ya bakteria ambayo yamekuwa sugu kwa viuavijasumu (antibiotics), kulingana na gazeti la Uhispania la El Pais.

Kwa msingi huo, vijidudu-maradhi hivyo vikubwa sasa vinaua watu wengi zaidi kuliko saratani, UKIMWI na malaria. Kwa mujibu ripoti hiyo, matokeo ya tafiti za jarida la matibabu la The Lancet zilizofanywa katika nchi 204, yanaonya kwamba idadi hii itaongezeka mara 10 zaidi kufikia mwaka 2050.

Wataalamu wa afya wanasema, katika chini ya miaka 30, vijidudu-maradhi vikubwa vitaua watu milioni 10 kwa mwaka, ikiwa ni mara tatu zaidi ya idadi inayokadiriwa ya vifo vilivyotokana na corona mnamo mwaka 2020.

Mmbu wanaosababisha malaria

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, mnamo mwaka 2019, karibu watu milioni moja na elfu 270 duniani walikufa kutokana  na maambukizi ya kawaida ya bakteria ambao wamekuwa sugu kwa viuavijasumu. Wahanga walikuwa ni wenyeji wa Asia Kusini, kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia Mashariki, Kusini-mashariki na Oceania, Amerika ya Latini na Karibian, Ulaya ya Kati, Ulaya Mashariki, Asia ya Kati na hatimaye Afrika Kaskazini na Asia Magharibi.

Jambo la kusikitisha ni kwamba hadi sasa hakuna tiba ya maambukizi hayo hatari.

Chanzo kikuu cha "tishio hili kubwa kwa afya ya binadamu ulimwenguni," kama wanavyosema waandishi wa utafiti huo muhimu, ni matumizi ya kupindukia ya viuavijasumu (antibiotics), tokea nusu ya pili ya karne iliyopita.