Jan 21, 2022 13:10 UTC
  • Papa Benedict XVI atuhumiwa kufifiliza unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto na makasisi wa Kanisa

Aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Benedict XVI ametuhumiwa kufifiliza na kuzembea katika kuchunguza matukio manne ya ripoti kuhusu ubakaji na unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto wadogo wakati yeye alipokuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Munich nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa ripoti, kiongozi huyo wa zamani wa kanisa katoliki amesema ameshtushwa na ripoti kuhusu unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto wadogo na makasisi nchini Ujerumani.

Halikadhalika, ripoti hiyo imemtuhumu Papa Benedict XVI, wakati huo akiwa Kadinali Joseph Ratzinger kwamba alizembea kuchunguza matukio manne ya ripoti ya kadhia hiyo wakati alipokuwa akiongoza Kanisa la Munich.

Makundi ya kutetea waathirika wa unyanyasaji wa kingono yamekaribisha na kupongeza kutolewa kwa ripoti hiyo na masuala yaliyobainishwa ndani yake.

Papa Benedict XVI alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Munich, Ujerumani kuanzia mwaka 1977 hadi 1982.

Katika kipindi hicho, kiongozi huyo wa kanisa alikataa kufanya chochote kuhusiana na unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto wadogo wanne na makasisi wa kanisa katoliki.

Ripoti iliyotolewa kuhusu kadhia hiyo imeeleza pia kwamba, akiwa na uelewa kamili, Papa Benedict XVI aliwaruhusu waendelee kufanya kazi kanisani, makasisii watatu ambao walithbitika kuhusika na vitendo hivyo.

Kiongozi huyo wa zamani wa kanisa katoliki anadai kuwa hakuwa na taarifa yoyote kuhusu rekodi za nyuma za makasisi hao, hata hivyo ripoti zinaonyesha kuwa kuna kikao kilifanyika kuwajadili makasisii hao, lakini Papa Benedict wa 16 anasema, yeye hakuhudhuria kikao hicho.

Makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican yametoa taarifa na kutangaza kuwa yatahakiki na kufanya uchunguzi kuhusu ripoti hiyo ya kurasa 1,700.  

Aidha Vatican imeeleza masikitiko yake kwa waathirika wa vitendo hivyo vya ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Kanisa Katoliki la Ujerumani limekuwa likitikiswa na ufichuzi kuhusu makasisi wanaolawiti watoto kwa zaidi ya miaka kumi. Theluthi mbili ya dayosisi imezindua tafiti, mara nyingi chini ya shinikizo kutoka nje.../                    

Tags