Jan 21, 2022 13:19 UTC
  • Wanafunzi Waislamu wapigwa marufuku kuvaa Hijabu katika chuo cha serikali India

Wanachuo Waislamu wanaovaa hijabu wamepigwa marufuku kuingia madarasani katika chuo cha serikali cha Udupi kilichoko kwenye jimbo la Karnataka kusini-magharibi ya India.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wafuasi wa misimamo ya chuki na kufurutu ada ya serikali ya waziri mkuu wa India Narendra Modi wanazidi kuongezeka, na kwamba baada ya kutolewa vitisho vya kuwaua Waislamu, sasa wasichana Waislamu wamezuiwa kuingia madarasani katika chuo cha serikali cha Udupi jimboni Karnataka kwa sababu tu wamevaa vazi la staha la Kiislamu la Hijabu.

Kwa muda wa mwezi mmoja sasa, chuo hicho kimewapiga marufuku wanafunzi Waislamu kuingia madarasani wakiwa wamevaa hijabu kwa kisingizio kwamba vazi hilo pamoja na kitambaa cha nikabu havimo kwenye orodha ya mavazi rasmi yanayokubalika kuvaliwa chuoni hapo.

Mmoja wa wanafunzi hao Waislamu ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia gazeti la The Indian Express; "tunaomba haki zetu za msingi; na si chengine chochote. Chuo kinajaribu kutoa taswira mbaya juu yetu kwa kudai haki zetu. Haturuhusiwi kuingia chuoni mpaka tuwe kama walivyo wanafunzi wengine. Zimeshafika siku 20 na tunahesabiwa kuwa hatuhudhurii darasani."

Tukio la wanafunzi Waislamu kupigwa marufuku kuvaa hijabu madarasani si la kwanza kuripotiwa katika miaka ya karibuni kwenye jimbo la Karnataka. Mbali na Udupi, matukio sawa na hayo yameripotiwa pia katika vyuo vya miji ya Dakshina, Kannada na Chikkamagaluru.../

Tags