Jan 22, 2022 02:39 UTC
  • Rekodi ya utendaji kazi ya Joe Biden, mwaka mmoja wa kuwa madarakani

Rais Joe Biden wa chama cha Democrat aliingia madarakani mwaka mmoja uliopita mnamo Januari 20, 2021, huku akitoa ahadi nyingi, hasa za kubadilisha hatua zilizochukuliwa na mtangulizi wake, Donald Trump, Rais wa zamani wa Marekani wa chama cha Republican.

Hivi sasa baada ya kupita mwaka mmoja tangu aingie madarakani, uungaji mkono wa Wamarekani kwa Joe Biden umepungua sana na utendaji wake ni wa kiwango cha chini kabisa, kadiri kwamba hata Wademocrat, ambao ni wafuasi wake wakubwa, hawana imani kuwa rais huyo atashinda uchaguzi ujao wa rais mwaka 2024. Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Morning Consult, asilimia 56 ya Wamarekani wanasema hawakubaliani na utendaji kazi wa Biden huku akiwa anaingia katika mwaka wake wa pili madarakani. Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa rais wa sasa wa Marekani ana uungaji mkono mdogo akilinganishwa na mtangulizi wake, Donald Trump, miaka minne iliyopita, na ni asilimia 40 pekee ya Wamarekani ndio wanaunga mkono utendaji kazi wake mwaka uliopita. Hii ni katika hali ambayo alipoingia madarakani tarehe 20 Januari mwaka uliopita, umashuhuri wake kwa mujibu wa Morning Consult, ulikuwa wa asilimia 50.

Biden anaingia katika mwaka wake wa pili madarakani katika hali ambayo mfumuko wa bei wa sasa nchini Marekani ulikuwa haujawahi kushuhudiwa katika miaka 43 iliyopita, ambapo umefikia zaidi ya asilimia 6.8. Katika hotuba aliyotoa ikulu ya White House mnamo Januari 7, mwaka huu, Biden alisema kwamba mfumuko wa bei nchini Marekani bado unatia wasiwasi, lakini kwamba njia ya kukabiliana nao sio kukwepa mipango ya kiuchumi. Warepublican wanasema mfumuko mkubwa wa bei wa hivi sasa nchini Marekani unatokana na mipango na sera za matumizi zinazotekelezwa na Biden.

Rais Joe Biden

"Mfumuko wa bei ni suala la kweli na tunapaswa kukabiliana nalo," alisema Tim Kaine, seneta wa chama cha Democrat kutoka jimbo la Virginia. Biden inataka kufufua uchumi wa Marekani ambao umeharibiwa vibaya na virusi vya Corona, kwa kuwasilisha mipango kadhaa ya kutoa msaada wa kifedha kwa familia za Marekani, kuongeza nafasi za kazi na kujenga upya miundombinu, ambayo itagharimu zaidi ya dola trilioni 6. Bila shaka, utawala wa Biden umefanikiwa kwa kiwango fulani katika kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira. Kuhusu siasa za ndani, Biden alijikita katika kurekebisha sheria za upigaji kura, lakini akashindwa kutokana na upinzani wa chama cha Republican katika bunge la Senate, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanaliona kuwa ni kushindwa kwingine kwa rais huyo wa Marekani.

Kwa upande mwingine, licha ya kutoa chanjo nyingi za kupambana na corona mwaka uliopita, lakini serikali ya Biden haijaonyesha suluhisho na utendakazi wa kuridhisha katika uwanja wa kuzuia kuenea nchini virusi vya corona na hasa katika kukabiliana na speshi mpya ya virusi hivyo yaani omicron.  Marekani kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya virusi vya corona na ina kiwango kikubwa zaidi cha magonjwa na vifo vinavyotokana na virusi hivyo duniani. Katika uwanja wa sera za uhamiaji pia, Biden licha ya kuahidi kubadilisha sera za Trump kuhusu suala hilo, lakini kivitendo vizingiti vingalipo na vitendo vya kinyama vinavyotekelezwa dhidi ya wahamiaji haramu vingali vinashuhudiwa, na la kushangaza hata zaidi ni kuwa anakusudia kuendelea kujenga ukuta wa mpakani ulioanzishwa na Trump.

Katika uga wa sera za kigeni pia, Biden umekuwa akifanya juhudi za kufufua muungano wa Bahari ya Atlantiki, ambao uliharibiwa vibaya wakati wa sera za upande mmoja za Trump ambazo ziliibua tofauti kubwa kati ya Marekani na Ulaya. Kwa upande mwingine, uhusiano wa Marekani na madola mawili hasimu ya kimataifa, China na Russia, umekuwa ukidorora na hali ya wasiwasi imeongezeka kati ya pande hizo mwaka uliopita. Utawala wa Biden umekuwa ukitoa madai na tuhuma nyingi zisizo na msingi dhidi ya Beijing na kusisitiza juu ya kutekeleza sera ya kuidhoofisha China. Mvutano na Russia pia umeongezeka kutokana na mzozo wa Ukraine, jambo ambalo limesababisha kuongezeka uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Ulaya.

Marekani imekuwa na mvutano wa muda mrefu na mahasimu wake, Russia na China

Pamoja na hayo yote, lakini fedheha kubwa zaidi aliyoipata Biden katika utekelezaji wa sera zake za kigeni ni suala la kuondoka kwa madhila jeshi la Merekani kutoka Afghanistan mnamo Agosti mwaka uliopita, jambo linalochukuliwa na wataalamu wa mambo kuwa ni ishara ya kudhoofika na kupungua nguvu ya kijeshi ya Marekani duniani. Utawala wa Biden ungali unafuata nyayo za utawala wa Trump katika kukabiliana na Iran na suala zima la makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, licha ya ahadi ulizotoa hapo awali kuwa ungetekeleza siasa tofauti katika uwanja huo. Washington pia imeshindwa kuboresha uhusiano wake na Korea Kaskazini na kuishawishi ianzishe tena mazungumzo ya pande mbili.

 

Tags