Jan 22, 2022 08:05 UTC
  • Sanders: Mfumo wa kisiasa wa Marekani ni bandia

Seneta mashuhuri wa Vermont amekosoa vikali sheria ya inayowaruhusu matajiri kufadhili wagombea katika chaguzi mbalimbali nchini Marekani.

Bernie Sanders amesema katika ujumbe wake wa Twitter kwamba."Mfumo bandia wa kiuchumi na kisiasa ni mfumo ambao mabilionea wametumia dola bilioni 1.2 kuwanunua wanasiasa katika kampeni za uchaguzi uliopita, na mabilionea hao wametajirika zaidi wakati wa janga la corona, na wanatoa ushuru mdogo sana kuliko hata wa muuguzi."

Seneta huyo wa Vermont alimetoa wito wa kufutwa sheria ya Citizen United inayoruhusu raia kufadhili wagombea katika chaguzi mbalimbali.

Chini ya sheria hiyo watu binafsi na mashirika yanaweza kufadhili kwa urahisi wagombea katika chaguzi za majimbo na za shirikisho.

Sheria hiyo ni sehemu ya juhudi za matajiri wa Marekani za kuwanunua wanasiasa ili kufikia malengo yao.

Hivi majuzi Bernie Sanders alisema kwamba, umri wa kuishi matajiri huko Marekani ni zaidi ya ule wa watu maskini kwa karibu miaka 15 .

Seneta huyo wa kujitegemea wa Vermont aliongeza, "Lazima tuwe na ujasiri wa kukabiliana na tamaa ya watendaji mabilionea na lobi zao. Mamilioni ya watu wameathiriwa na pengo hili la kimatabaka, na wakati huo huo, matajiri wana maisha bora zaidi kuliko hapo awali."

Hali mbaya ya makumi ya mamilioni ya Wamarekani katika suala la umaskini, ukosefu wa makazi na njaa, pamoja na kukosa uwezo wa kugharamia matibabu, ni ishara ya hali mbaya ya kimfumo katika nchi hiyo inayodai kuwa nchi ya kibepari iliyoendelea zaidi duniani.