Jan 23, 2022 02:37 UTC
  • Indhari ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu ukosefu wa ajira nchini Afghanistan

Shirika la Kazi Duniani (ILO) limetahadharisha kuhusu kuendelea ukosefu wa ajira miongoni mwa wananchi wa Afghanistan.

Taarifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) imeeleza kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wamepoteza ajira zao katika miezi ya karibuni na kwamba mwenendo huo umeisababisha jamii ya nchi hiyo matatizo mengi. Ukosefu wa kazi unaowakabili wananchi wa Afghanistan kwa maana ya kukosa ajira wanawake na wanaume wa nchi hiyo unasababishwa na masuala mawili yafuatayo. Kwanza ni kuwa, kundi la wanamgambo wa Taliban ambalo kwa mara nyingine tena liliingia madarakani tangu mwezi Agosti uliopita limepiga marufuku au kuzuia shughuli mbalimbali zikiwemo zile ambazo zilikuwa zikifanywa na wanawake nchini humo; na sasa wananchi wa Afghanistan wameathiriwa na mdodoro wa kiuchumi  kwa kuzingatia vizuizi na marufuku zilizowekwa na kundi hilo. Miongozi mwa vizuizi na marufuku hizo za Taliban tunaweza kuashiria vile vilivyowekwa kwa vyombo vya habari, ambapo katika miezi ya hivi karibuni Afghanistan imeathirika pakubwa na kuporomoka hali ya kiuchumi.   

Utawala wa kundi la Taliban 

Pili ni kwamba, hali ya ukosefu wa ajira nchini Afghanistan imesababishwa na nchi zilizoivamia nchi hiyo ambazo zimepuuza suala la kuijenga upya nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita na machafuko sambamba na kutoandaa vyanzo vipya vya kiuchumi na kiviwanda; jambo linalorejea nyuma miongo miwili iliyopita; ambapo kwa kusambaratika serikali za kiliberali nchini humo imebainika wazi kwamba Afghanistan haina miundomsingi yoyote ya kiuchumi na kiviwanda. 

Hakuna shaka kuwa kukosa shughuli za kufanya zaidi ya nusu ya jamii ya watu wa Afghanistan kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kumeiathiri vibaya nchi hiyo  kijamii na kiusalama. 

Kuongezeka umaskini na njaa kumesababisha watoto huko Afghanistan kuathiriwa na utapiamlo, kushuhudiwa vitendo vya wizi na uporaji na kuongezeka aina mbalimbali ya magendo; yote hayo yakiwa ni athari za kuongezeka ukosefu wa ajira nchini. Hali hiyo ambayo imesababishwa na duru za Magharibi imeharibiwa zaidi na Marekani ambayo inaendelea kuwazidishia masaibu na matatizo wananchi wa Afghanistan kwa hatua yake ya kuzuia fedha za watu wa nchi hiyo. Ndio maana Umoja wa Mataifa hivi karibuni ukazitaka Marekani na nchi nyingine za Magharibi kuachia fedha hizo tajwa za wananchi wa Afghanistan ili kuupatia ufumbuzi mgogoro unaowakabili Waafghanistan.  

Uvamizi wa nchi ajinabi nchini Afghanistan 

Ala kulli hal, kundi la Taliban ambalo linatambua vyema kuwa linahusika na hali hiyo ya mambo ya wananchi wa Afghanistan linaweza kusaidia kurekebisha hali hiyo kwa kuwaandalia nafasi za ajira watu wa nchi hiyo iwapo litalegeza na kuachana na misimamo na siasa zake kali zisizo na msingi.  

Kundi la Taliban ambalo limewataka raia wa Afghanistan waliohamia katika nchi jirani kurejea nyumbani linahitajia kwanza kuandaa nafasi za ajira ili kuhuisha shughuli mbalimbali za kiviwanda na kwa njia hiyo wale waliobobea katika fani mbalimbali  katika nchi jirani pia waweze kuwa na mchango katika maendeleo ya kiviwanda ya Afghanistan. 

Tags