Jan 23, 2022 02:40 UTC
  • China yasema Marekani ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia

China imetahadharisha kuwa Marekani ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia kutokana na maghala yake makubwa ya silaha angamizi za nyuklia.

Katika taarifa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amesema Marekani ina maghala makubwa zaidi ya silaha za nyuklia duniani na hivyo nchi hiyo ni tishio kwa usalama wa dunia. Ameendelea kusema kuwa: "Kama sote tunavyojua, Marekani ni tishio kubwa zaidi kwa uthabiti wa dunia kwani inamiliki ghala la silaha za kisasa kabisa za nyuklia."

Ameongeza kuwa, Marekani imesambaza makombora yake kote duniani na kuongeza kuwa, "Pamoja na kuwa Marekani inamiliki idadi kubwa na ya kisasa kabisa ya silaha za nyuklia, lakini ingali inawekeza matrilioni ya dola kuboresha silaha za nyuklia huku ikijiondolea masharti magumu ya kutumia silaha hizo"

Zhao Lijian pia ameitaka Marekani ishughulikie masuala yanayoihusu kabla ya kuanza kuikosoa China na pia ipunguze silaha zake za nyuklia ili hatua hiyo iwe mfano kwa nchi zingine. Amesema China inazingatia sera ya nyuklia ya kujihami na pia inafungamana na sera ya kutokuwa nchi ya kwanza inayotumia silaha za nyuklia vitani.

Moja ya maghala ya maelfu ya mabomu ya nyuklia ya Marekani

Kauli hiyo imekuja baada ya Marekani na Japan kutoa taarifa mnamo Januari 20 ambapo zilibainisha wasiwasi wao juu ya kile zilichodai kuwa ni 'ongezeko la uwezo wa kinyuklia wa China." Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema taarifa hiyo haina ukweli wowote.

 

Tags