Jan 23, 2022 07:56 UTC
  • Kamanda wa jeshi la wanamaji la Ujerumani ajiuzulu kwa 'kuikingia kifua' Russia

Kamanda wa kikosi cha wanamaji cha jeshi la Ujerumani Admeri Kay-Achim Schoenbach amejiuzulu wadhifa wake baada ya matamshi aliyotoa kwamba "eneo la Crimea katu halitarejea tena mikononi mwa Ukraine" kuzusha makelele ndani ya nchi hiyo na katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Admeri Kay-Achim Schoenbach, alinukuliwa katika kikao cha jopo la wanafikra kilichofanyika siku ya Ijumaa katika taasisi ya mitaala na uhakiki wa kiulinzi ya  Manohar Parrikar nchini India akihoji: "Ni kweli Russia inautaka ukanda mdogo na mwembamba wa ardhi ya Ukraine au kuunganisha na nchi yake? Hapana, ni upuuzi tu. Yamkini Putin anatoa mashinikizo, kwa sababu anajua anaweza kufanya hivyo na kuleta mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya... lakini anachokitaka hasa ni heshima ya kiwango cha juu. Ni rahisi kumpa heshima anayoitaka na pengine anastahiki."

Wakazi wa Crimea wakisherehekea eneo lao kuunganishwa na ardhi ya Russia

Kuhusiana na uamuzi wake wa kujiuzulu, Schoenbach, amesema, amemuomba waziri wa ulinzi Christine Lambrecht  amwondoe katika wadhifa wake kupitia utaratibu wa uchukuaji hatua ya haraka na kwamba waziri huyo amelikubali ombi lake.

Uhusiano wa Magharibi na Russia umeharibika na kuingia kwenye duru ya mivutano na mikwaruzano tangu mwaka 2014 baada ya eneo la Peninsula ya Crimea la ardhi ya Ukraine kuunganishwa na Russia.

Mivutano hiyo imeshadidi hivi karibuni baada ya Marekani na waitifaki wake wa Ulaya kuituhumu Russia kuwa ina mpango wa kuivamia kijeshi Ukraine, madai ambayo Kremlin imeyakanusha.../