Jan 23, 2022 12:20 UTC
  • Watetezi wa haki za wanawake nchini Ufaransa wapinga marufuku ya hijabu michezoni

Watetezi wa haki za wanawake nchini Ufaransa wamepinga vikali mpango uliopasishwa hivi karibuni na Baraza la Seneti la nchi hiyo ya bara Ulaya unaopiga marufuku uvaaji wa vazi la staha na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo.

Watetezi wa haki za wanawake nchini Ufaransa wamesema kuwa, wanapinga vikali mpango huo ambao unawazuia wanawake Waislamu kuvaa vazi la stara ya mwanamke wa Kiislamu hijabu katika mashindano ya michezo.

Wiki iliyopita, Baraza la Seneti la Ufaransa lilipiga kura na kupasisha sheria inayopiga marufuku uvaaji wa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo.

Hatua hiyo ambayo ni muendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu inatarajiwa kuzusha makelele na malalamiko mengi wakati mji mkuu wa Ufaransa Paris unatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki mwaka 2024.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, endapo marufuku hiyo itajumuisha mashindano ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Parsi mwaka 2024 huenda yakayafanya mashindano hayo kukabiliwa na changamoto kubwa.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia)

 

Hii ni kutokana na kuwa, kama wanamichezo Waislamu watasusia mashindano hayo itakuwa pigo kubwa hasa kwa kuzingatia kuwa, katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020 wanamichezo Waislamu walikuwa na nafasi na hisa kubwa ya medali katika mashindano hayo.

Huko nyuma pia Baraza la Seneti la Ufaransa limewahi kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.

Tangu Rais Emmanuel Macron aliposhika hatamu za uongozi nchini Ufaransa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kuvunjiwa heshima matukufu ya  Uislamu vimeongezeka mno katika nchi hiyo ya bara Ulaya.