Jan 24, 2022 02:41 UTC
  • 80% ya Wamarekani: Ugaidi wa ndani ni tishio kubwa kwa Marekani

Akthari ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa, ugaidi wa ndani ya nchi ni tishio kubwa kwa taifa hilo.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na jarida la The Economist kwa ushirikiano na kampuni ya utafiti ya YouGov, zaidi ya asilimia 80 ya Wamarekani wanaitakidi kuwa, ugaidi wa ndani ya nchi ni tishio kubwa kwa Marekani.

Aidha utafiti huo umeonesha kuwa, asilimia 50 ya wananchi wa Marekani waliohojiwa wanaamini kuwa, magenge ya wabeba silaha wa mrengo wa kulia ni tishio kubwa la hivi sasa kwa jamii ya Wamarekani.

Hata hivyo matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa na gazeti la The Hill yameonesha kuwa, asilimia 66 ya Wamarekani wanaamini kuwa, magenge hayo ni tishio kubwa, lakini si katika kipindi hiki cha sasa.

Watu 1,500 wameshirikishwa kwenye utafiti huo wa maoni uliofanyika katikati ya mwezi huu wa Januari, mwaka mmoja baada ya tukio la kuvamiwa Kongresi ya Marekani na wafuasi sugu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump. 

Hujuma dhidi ya Kongresi ya US

Kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika Januari 6 mwaka jana kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 huko Marekani, kilikabiliwa na shambulio la wafuasi wa Trump na kusimama kwa masaa kadhaa. 

Watu wasiopungua watano wakiwemo maafisa usalama waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa, katika shambulio hilo la Wamarekani wenye misimamo ya kuchupa mipaka (White Supremacists).   

Tags