Jan 24, 2022 02:41 UTC

Seneta mmoja mashuhuri huko Marekani amesema kitendo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump cha kujitoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ndio uamuzi wa kipumbavu zaidi katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Chris Murphy, ambaye pia ni mwanachama wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni wa Seneti ya Marekani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa, mbali na uamuzi huo wa Trump kuwa wa kipumbavu zaidi, lakini pia ndio uamuzi hatari zaidi kwa sera za kigeni za Marekani ndani ya miongo mitano iliyopita.

Seneta huyo ameeleza bayana kuwa, uamuzi huo wa upande mmoja wa Trump wa Mei mwaka 2018, ulipingwa vikali na hata maafisa wa karibu wa utawala uliopita Marekani, wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ulinzi.

Wiki iliyopita pia, viongozi wa Ikulu ya Marekani, White House walisema kitendo hicho cha Trump cha kujitoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa, lilikuwa ni kosa kubwa kutokana na rais huyo wa zamani wa Marekani kutokuwa na ratiba zozote za kukabiliana na yatakayotokea baada ya kujitoa kwake.

Seneta Murphy (kushoto) na Trump

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya sasa Marekani inayoongozwa na Joe Biden sambamba na kukiri kufeli vikwazo vya kiwango cha juu kabisa ambazo Donald Trump aliiwekea Iran, imedai kuwa itarejea kwenye mapatano ya JCPOA, ingawa hadi hivi sasa White House haijachukua hatua yoyote ya maana ya kufanikisha madai hayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, itatekeleza kikamilifu vipengee vyote vya makublaiano ya JCPOA iwapo tu Marekani itaondoa vikwazo vyote vya kidhulma ilivyoliwekea taifa la Iran na baada ya Tehran kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa kweli Washington imeondoa vikwazo hivyo.

Tags