Jan 24, 2022 08:11 UTC
  • Alliyejificha katika tairi la ndege akutwa hai baada ya ndege kutua Uholanzi ikitokea Afrika Kusini

Maafisa nchini Uholanzi wamemkuta akiwa hai mtu mmoja aliyekuwa amejificha katika tairi la ndege ya mizigo wakati ilipotua jana asubuhi katika uwanja wa ndege wa Schiphol huko Amsterdam.

Ndege hiyo ya mizigo ilikuwa ikitokea Afrika Kusini kuelekea Ulaya; ambapo imeelezwa kuwa ilitua kwa muda nchini Kenya kabla ya kuendelea na safari hadi Amsterdam Uholanzi.  

Mtu huyo ambaye uraia, jinsia na umri wake bado havijafahamika sasa yuko hospitalini akiendelea kuangaliwa afya yake. 

Msemaji katika uwanja wa ndege wa Schiphol mjini Amsterdam na polisi wamesema kuwa, mwanaume huyo aliyezamia  alijificha katika tairi la ndege ya mizigo kwa muda wa masaa 11 tangu iruke kutoka Johannesburg Afrika kusini. Mtu huyo anaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 16 hadi 35.

Uwanja wa ndege wa Nairobi, JKIA

Willemeike Koster Msemaji wa uwanja huo wa ndege amesema kuwa walipata taarifa ya kukukutwa mtu huyo katika  ndege hiyo ya mizigo na kwamba polisi wanaendelea kufuatilia kadhia hiyo. Ameongeza kuwa, wameshtushwa na mtu huyo kusalia hai baada ya ndege kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita elfu kumi tena katika baridi kali sana. 

Itakumbukwa kuwa mwaka 2019 mtu mmoja aliyesadikiwa kuwa alizamia kwenye ndege ya Kenya Airways iliyokuwa ikitokea Nairobi alianguka dakika chache kabla ya ndege hiyo kutua Uwanja wa Ndege wa Heathrow mjini London. Mwili wa mzamiaji huyo ulipatikana katika bustani ya Clapham.