Jan 24, 2022 12:26 UTC
  • Nusrat Ghani
    Nusrat Ghani

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameamuru uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya waziri wa zamani Muislamu aliyesema kwamba alifutwa kazi katika serikali yake kwa sababu ya imani yake ya Kiislamu.

Madai hayo yaliyotolewa na Nusrat Ghani, aliyekuwa waziri mdogo wa uchukuzi, yamezua utata mpya huko Downing Street huku Boris Johnson akisubiri matokeo ya uchunguzi mwingine kuhusu kashfa ya "partygate".

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza amesema leo Jumatatu kwamba "Boris Johnson ameitaka Ofisi ya Baraza la Mawaziri kufanya uchunguzi kuhusu madai yaliyotolewa na Mbunge Nusrat Ghani."

Ghani amekaribisha uchunguzi huo mpya ambao ulitangazwa baada ya kufanya mazungumzo na Boris Johnson Jumapili jioni.

Nusrat Ghani, 49, alifutwa kazi kama waziri wa uchukuzi mnamo 2020, na ameliambia gazeti la Sunday Times kwamba "Uislamu wake ulijadiliwa" katika mkutano uliofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu, Downing Street.

Nusrat Ghani

Pia aliambiwa kwamba "hadhi yake ya kuwa waziri mwanamke wa Kiislamu ilikuwa ikiwafanya wenzake wajisikia vibaya".

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekuwa akilaumiwa kwa kuwa na misimamo inayopinga Uislamu na kuchukia Waislamu. 

Mwaka 2018, Johnson alikosolewa vikali kwa kuandika kwamba, wanawake wa Kiislamu waliovaa burqa wanaonekana kama "sanduku za barua" na "wezi wa benki".

Tags