Jan 24, 2022 12:28 UTC
  • ICN yatahadharisha kuhusu ukosefu wa usawa katika sekta ya afya zama za corona

Baraza la Kimataifa la Wauguzi (ICN) limeonya juu ya kuongezeka harakati ya kuajiri wauguzi kutoka nchi maskini kwenda nchi tajiri huku aina ya Omicron ya kirusi cha corona ikiongezeka katika nchi hizo.

Baraza la Kimataifa la Wauguzi limetangaza kwamba wimbi kubwa la maambukizi ya Omicron limelazimisha nchi tajiri kuajiri wauguzi kutoka nchi maskini zaidi, suala ambalo limeongeza uhaba wa wafanyakazi katika nchi zenye kipato cha chini.

Howard Catton, mkurugenzi wa baraza hilo lenye makao yake Geneva huko Uswisi, ambalo linawakilisha wauguzi milioni 27 na mashirika ya kitaifa 130 amesema: "Ugonjwa, uchovu na kuacha kazi baadhi ya wauguzi katika kilele cha mlipuko wa Omicron vimezidisha uhaba mkubwa wa wauguzi ambao haujawahi kushuhdiwa wakati wa janga la corona."

Catton ameongeza kuwa, ili kuziba pengo hilo, nchi za Magharibi zinaajiri wanajeshi, wafanyakazi wa kujitolea na waliostaafu, na baadhi ya nchi zimezidisha harakati za kuwaajiri wauguzi wa kigeni jambo ambalo linazidisha pia ukosefu wa usawa katika sekta ya afya.

Uhaba wa wauguzi katika nchi maskini

Nchi zinazoongoza katika uwanja huu ni Marekani, Uingereza, Canada na Ujerumani.

Kulingana na Baraza la Kimataifa la Wauguzi, hata kabla ya kuibuka janga la Covid-19, kulikuwapo uhaba wa wauguzi milioni 6 duniani, na karibu asilimia 90 ya uhaba huo unashuhudiwa katika nchi zenye kipato cha chini.

Tags