Jan 25, 2022 02:28 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Mifumo ya elimu imepitwa na wakati, kuna haja ya kuirekebisha

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa, janga la COVID-19 na changamoto nyingine zinazoikabili dunia hivi sasa zimedhihirisha umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa ya ulimwengu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Elimu Duniani iliyoadhimishwa kote ulimwengu jana tarehe 24 Januari na kiubainisha kwamba, “dunia yetu inabadilika kwa kasi ya haraka mno, ubunifu katika teknolojia, mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye dunia ya ajira, dharura ya mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa ukosefu wa imani baina ya watu na taasisi.”

Guterres ameongeza kuwa, mifumo ya kawaida ya elimu inahaha kutoa elimu, stadi na maadili ambayo ni lazima kuijenga ili kuweko na mustakabali bora, salama na unaojali mazingira kwa wote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametolea mfano wa janga la Corona akieleza kwamba, limetibua sekta ya elimu duniani kote.

Shule nyingi duniani zimefungwa kutokana na kusambaa virusi vya Corona

 

Takribani wanafunzi bilioni 1.6 wa Vyuo Vikuu na shule masomo yao yalivurugika wakati janga  la Corona lilipoanza  tu na hadi sasa bado halijaisha ambapo hii leo, ufungaji wa shule unaendelea kuvuruga maisha ya mamilioni ya wanafunzi milioni.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, “tusipochukua hatua, idadi ya watoto wanaoacha shule katika nchi zinazoendelea na ambao hawajui kusoma na kuandika inaweza kuongezeka kutoka asilimia 53 hadi asilimia 70.”