Jan 25, 2022 07:46 UTC
  • Biden amtusi mwanahabari aliyemuuliza swali kuhusu mfumko wa bei

Rais Joe Biden wa Marekani ameendelea kushambuliwa hususan katika mitandao ya kijamii kwa kitendo chake cha kumtukana vibaya mwandishi mmoja wa habari ambaye alimuuliza suali kuhusu mfumko wa bei za bidhaa unaoshuhudia nchini humo.

Biden alinaswa akimtusi matusi ya nguoni ripota wa televisheni ya Fox News katika Ikulu ya White House, ambaye alikuwa anatekeleza wajibu wake wa kuuliza maswali mazito kuhusu sera za uchumi za Biden, kwa niaba ya Wamarekani.

Rais huyo wa Marekani ambaye alidhani kuwa kipaza sauti kilikuwa kimeziwa wakati akijibu suali hilo, amemuita Peter Doocy, mwandishi huyo wa habari wa Fox News 'mpumbavu na mwanaharamu'.

Kutokana na mashinikizo na ukosoaji mkali hususan kwenye vyombo vya habari na mtandao wa kijamii wa Twitter, Biden amelazimika kumpigia simu mwanahabari huyo na kumuomba radhi.

Weledi wa mambo wanasema, hivi sasa baada ya kupita mwaka mmoja tangu aingie madarakani, uungaji mkono wa Wamarekani kwa Biden umepungua sana, na utendaji wake ni wa kiwango cha chini kabisa, kadiri kwamba hata Wademocrat, ambao ni wafuasi wake wakubwa, hawana imani kuwa rais huyo atashinda uchaguzi ujao wa rais mwaka 2024.

Trump na Biden

Mtangulizi wa Biden, Donald Trump aliwahi pia kuwatukana vibaya waandishi wa habari, na hata kuviita 'ghushi' vyombo vya habari vilivyokuwa vikimkosoa akiwa uongozini.

Hii ni katika hali ambayo, Marekani kwa miongo mingi sasa imekuwa ikizivamia nchi nyingine duniani kwa kutumia 'silaha' ya demokrasia na uhuru ukiwemo uhuru wa vyombo vya habari.

Tags