Jan 27, 2022 02:37 UTC
  • Marekani yaendelea kuiuzia Misri silaha licha ya faili lake jeusi la haki za binadamu

Marekani imeidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 2.5 kwa Misri licha ya serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuendelea kuandamwa na shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu.

Utawala wa Rais Joe Biden umeidhinisha mauzo hayo ya silaha kupitia taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa, Washington itaiuzia Cairo ndege 12 za kijeshi aina ya C-130J-30 Super Hercules zenye thamani ya dola bilioni 2.2.

Imeongeza kuwa, katika mauzo hayo, Marekani imekubali kuiuzia Misri mifumo mitatu ya rada ya ardhini aina ya SPS-48, kwa thamani ya dola milioni 355.

Washington inadai kuwa, mauzo haya mapya ya silaha ya mabilioni ya dola hayana mfungamano wowote na msaada wa kijeshi wa dola milioni 130 ambao ulisimamishwa mwezi Septemba mwaka jana, kutokana na Misri kutofikia kiwango fulani cha kuheshimu haki za binadamu.

Rais Sisi anayeshutumiwa kwa kukanyaga haki za Wamisri

Marekani imeidhinisha mauzo hayo katika hali ambayo, serikali ya Abdel Fattah el Sisi wa Misri kwa miaka mingi sasa imekuwa ikikosolewa vikali na mashirika ya kitaifa na kimataifa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimetoa indhari kuhusu utendaji wa utawala wa Misri unaoongozwa na Sisi katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Tags