Jan 27, 2022 10:48 UTC
  • Makaburi ya siri yagunduliwa katika shule ya kanisa Canada

Makaburi ya siri yagunduliwa katika uwanja mmoja uliokuwa unamilikiwa na kanisa katoliki nchini Canada.

Baraza la William Lake First Nation katika eneo la British Columbia nchini Canada limesema uchunguzi wa awali katika shule ya bweni ya Misheni ya St Joseph inayomilikiwa na Kanisa Katoliki umebaini kuwa kuna makaburi katika eneo la uwanja wa shule hiyo.

Chifu Willie Sellars wa eneo hilo amesema uchunguzi umebaini kuwepo makaburi ambayo yanaashiria kutendeka jinai.

Shule hiyo ya bweni ya Kanisa Katoliki huko British Columbia ambayo ilifunguliwa 1891 na kufungwa 1981 ina historia chafu ya udhalilishaji wanafunzi ambao wote walikuwa wakaazi asilia Wahindi wa Canada. Wanafunzi wengi waliokuwa katika shule hiyo walilazimika kutoroka huku wengine wakijaribu kujiuzua na wengine wakifariki wakati wa kutoroka.

Watu wa jamii asilia ya Canada wakikumbuka watoto wao waliouawa kwa umati katika shule ya kanisa katoliki

Uchunguzi wa kutafuta makaburi ya umati ya wakazi asilia wa Canada ulianza mwishoni mwa mwezi Mei mwaka jana baada ya kugunduliwa mabaki ya maiti 215 za wanafunzi wa shule ya bweni ya kikatoliki ya Kamloops Indian katika jimbo la British Columbia iliyofungwa mnamo 1978. Mtandao wa gazeti la The National Post la Canada uliripoti kwamba, kumegunduliwa mamia ya makaburi ambayo hayajasajiliwa katika mkoa wa Saskatchewan ambayo yanadhaniwa yana maiti za watoto waliokuwa wakishikiliwa katika shule nyingine ya bweni ya wamishonari wa Kikatoliki. Makaburi hayo ambayo hayana alama yoyote yana maiti za watoto 751. Kugunduliwa makaburi hayo kumezusha mshtuko mkubwa nchini Canada na maeneo mengine ya dunia. Kwa sasa zinafanyika jitihada za kusaka makaburi mengine ya aina hiyo.  

Rosanne Casimir ambaye ni mkuu wa mojawapo ya makabila ya mji wa Kamloops katika jimbo la British Columbia alisema baada ya kugunduliwa makaburi hayo mwaka jana kwamba: "Vifo vya watoto hao wa wakazi asilia wa Canada havikusajiliwa katika waraka wowote wa shule, na suala hili pekee ni ushahidi kwamba, maafisa na viongozi wa shule hizo walihusika katika vifo vya watoto hao."

Kuanzia mwaka 1883 hadi 1996 zaidi ya watoto laki moja na nusu wa wakazi asilia wa Canada walilazimishwa kuishi katika shule makhsusi zilizokuwa zikisimamiwa na wamishonari na wahubiri wa Kikatoliki ili eti kuwaingiza katika jamii ya Canada.