Jan 27, 2022 11:05 UTC
  • Iran: Mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa kukiwa na wavamizi wa kigeni

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya kijitawala Syria ambao unatekelezwa na askari vamizi wa kigeni na magaidi na kusema, mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo hauwezi kutatuliwa iwapo kutaendelea kuwepo nchini humo wavamizi wa kigeni.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht-Ravanchi aliyasema hayo Jumatano katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya mambo Asia Magharibi  na kuongeza kuwa: "Mamlaka ya kujitawala na ardhi ya Syria inaendelea kukiukwa kupitia kukaliwa kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo au kuvamiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na magaidi."

Ameendelea kusema, "pamoja na kuwa mgogoro wa Syria hauna utatuzi wa kijeshi lakini mgogoro huo hauwezi kumalizika maadamu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yanakaliwa kwa mabavu."

Aidha amesisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na tishio la kigaidi Syria na ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema ukaliaji mabavu, uvamizi na vikwazo vilivyo dhidi ya ubinadamu ni mambo ambayo yamepelekea watu wa Syria waendelee kukumbwa na masaibu huku akisisitiza kuwa askari wa kigeni ambao hawajaalikwa na serikali ya nchi hiyo lazima waondoke.

Milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel

Aidha ametoa wito kwa Baraza la Usalama kulaani mkutano wa kichochezi wa baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Syria ya Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Israel ilikalia kwa mabavu milima hiyo mwaka 1967.

Disemba mwaka jana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio linalolaani hatua zote za Israel katika eneo la Syria la Golan linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo na kuutaka utawala wa Kizayuni ukomeshe hatua zote zinazokiuka sheria za kimataifa.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisisitiza kuwa, hatua zilizochukuliwa na zitakazochukuliwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kubadili utambulisho na hali ya kisheria ya eneo la Golan la Syria ni batili na zinakiuka kanuni na sheria za kimataifa.