Jan 28, 2022 01:39 UTC
  • Vyombo vya habari vya Russia: Marekani na Uingereza zinaiuzia Ukraine silaha zilizochakaa

Vyombo vya habari vya Russia vimeripoti kuwa, Marekani na Uingereza zinaiuzia Ukraine silaha na zana za kijeshi zilizochakaa na za zamani sana.

Televisheni ya Russia 24 imeripoti kuwa, Valery Ignatenko mbunge wa Ukraine ameeleza kuwa Marekani inatuma Ukraine silaha zilizochakaa sana. Ameongeza kuwa, silaha ambazo tayari zimetumwa hivi sasa nchini humo ni zile za muongo wa 80.

Hadi kufikia sasa Marekani imetuma nchini Ukraine shehena tatu za silaha na zana za kijeshi pamoja na ndege za jeshi za usafiri. Kiujumla karibu tani 250 za silaha zimekabidhiwa Ukraine hadi sasa.

Silaha zilizochakaa kutoka Marekani na Uingereza kuelekea Ukraine 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Uingereza pia nayo imetumia fursa iliyojitokeza kufuatia mivutano ya hivi karibuni kuhusu Ukraine na kutuma ndege kadhaa za kijeshi za usafirishaji aina ya Boeing zilizosheheni aina mbalimbali za silaha kwa ajili ya Ukraine. 

Uhusiano wa nchi za Magharibi na Moscow ulivurugika tangu mwaka 2014 kutokana na mambo kadhaa ikiwa ni kupanua ushawishi wa kijeshi Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) khususan Marekani karibu na mipaka ya Russia na huko Ulaya mashariki, mgogoro wa Ukraine, kadhia ya Bahari ya Baltic na mgogoro wa Syria.   

Russia nayo kwa upande wake imeeleza waziwazi kwamba kuwepo kwake kijeshi katika mpaka kati ya nchi hiyo na Ukraine na jambo la kawaida. Hata hivyo Marekani na waitifaki wake zinafanya kila ziwezalo ili kuidhihirisha hali ya mambo katika mpaka wa Russia na Ukraine kuwa ni ya mvutano.  

Tags