Jan 29, 2022 02:56 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa kisiasa dhidi ya waziri mkuu wa Uingereza

Kufuatia kufichiliwa habari ya uwezekano wa ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza kuvunja kanuni na sheria za corona, polisi ya nchi hiyo imeanzisha uchunguzi wa kubaini ukweli wa jambo hilo.

Kufuatia kuenea virusi vya corona huko Uingereza na kama ilivyokuwa katika nchi nyingine za dunia, serikali ya London iliweka kanuni na sheria za kuzuia mikusanyiko ya kijamii ikiwemo mialiko na sherehe za watu binafsi na kuanisha hatua za kisheria ambazo zingechukuliwa dhidi ya wahalifu wa sheria hizo.

Gazeti la Guardian siku chache zilizopita lilichapisha picha ya Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, akiwa na makumi ya watu kwenye bustani ya makazi ya waziri mkuu katika Jengo nambari 10, Downing Street, ambao kwa mujibu wa gazeti hilo, walishiriki kwenye karamu iliyoandaliwa mwezi Mei 2020 wakati wa kutekelezwa karantini na marufuku ya corona.

Kufichuliwa habari hiyo kumeibua mzozo na mjadala mkubwa huko Uingereza katika wiki kadhaa zilizopita, mjadala ambao umehatarisha nafasi ya kisiasa ya Waziri Mkuu pamoja na chama chake tawala cha Wahafidhina. Siku kadhaa zilizopita, Keir Starmer , Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour alimtaka Waziri Mkuu Boris Johnson ajiuzulu mara moja kutokana na kashfa hiyo. Huku akisema kuwa hatua hiyo ya Waziri Mkuu imepelekea kupungua imani ya Waingereza kwake na hivyo kudhoofisha utendaji kazi wake, Starmer amesisitiza kuwa kuondolewa Waziri Mkuu Johnson katika nafasi hiyo kutakuwa na mafuu kwa nchi hiyo.

Boris Johnson

Kuongezeka ukosoaji dhidi ya Boris Johnson kumepelekea pia kupungua uungaji mkono wa raia wa Uingereza kwake na kwa chama tawala. Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa karibuni nchini Uingereza, uungaji mkono wa Waingereza kwa chama tawala umepungua na kufikia kiwango cha asilimia 42 pekee.

Kufichuliwa habari ya kuandaliwa karamu na sherehe katika makazi ya waziri mkuu katika jengo nambari 10 ambayo sasa inajulikana kama kashafa ya 'Partygate' kumemlazimisha waziri mkuu huyu awaombe radhi Waingereza na kuwafuta kazi mawaziri kadhaa ili kutuliza hasira yao lakini hadi sasa hatua yake hiyo haijakuwa na natija yoyote chanya kwake, bali hata imeharibu zaidi hali ya mambo.

Katika kujibu maswali ya wabunge, Boris Johnson amejitetea kwa kudai kwamba karamu hiyo ilikuwa ni ya kikazi na kwamba ilifanyika kisheria. Wakati huohuo, Dominic Cummings, mshauri mkuu wa zamani wa Boris Johnson amemtuhumu waziri mkuu huyo kwa kusema uongo na kusisitiza kuwa tangu mwanzo alifahamu vizuri kuwa angeshiriki katika karamu na mwaliko huo.

Huku akisisitiza kuwa kuomba msamaha kulikofanywa na Waziri Mkuu hakutoshi, Keir Starmer, Kiongozi wa Chama cha Lebour amesema kuwa msamaha alioomba waziri mkuu huyo kwenye bunge ni dharau na kejeli kwa taifa la Uingereza. William Wragg, mwenyekiti wa kamati inayoshughulikia masuala ya uongozi wa serikali na katiba na ambaye pia ni mwanachama wa Chama tawala cha Conservative, amesema kuwa atamshtaki Johnson kwa tuhuma ya kutisha na kuwatia hofu wanachama wa Bunge.

Hii ni katika hali ambayo wafuasi wa Johnson wanasema huu sio wakati mwafaka wa kumtimua madarakani waziri mkuu wa Uingereza. Ndio maana Waziri wa Ulinzi wa Uingereza James Hippie akawataka wenzake wa chama cha Conservative au Wahafidhina watumie busara katika kukabiliana na kashfa hii ya kisiasa.

Keir Starmer, Kiongozi wa Chama cha Lebour

Lakini kwa kuwa sasa polisi ya London imeingilia kati kwenye kesi hiyo ya karamu yenye utata ya Waziri Mkuu, mzozo wa kisiasa dhidi ya Johnson unaendelea kuwa mkubwa siku baada ya nyingine.

Roger Gill, mbunge wa Wahafidhina wa Uingereza amesema kuhusu kashfa hiyo kwamba: "Kwa hakika Johnson tayari ni maiti ya kisiasa inayotembea."

Hii ni katika hali ambayo, iwapo serikali ya Johnson itaanguka huku mzozo wa Ukraine ukiwa umezikumba nchi za Magharibi na taifa hilo la tano kwa ukubwa kiuchumi duniani likipambana na wimbi kubwa la mfumuko wa bei na kuendelea kwa janga la corona,  ni wazi kuwa hali hiyo itaiweka Uingereza katika hali ya mashaka na isiyojulikana vyema kwa muda mrefu.