Jan 29, 2022 08:16 UTC
  • Troika ya Ulaya: Tunakaribia hatua ya mwisho katika mazungumzo ya Vienna

Wawakilishi wa nchi tatu za Ulaya katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo yanayofanyika mjini Vienna wamesema, mazungumzo hayo yanakaribia awamu ya mwisho na yanahitaji maamuzi ya kisiasa.

Wanadiplomasia wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wametangaza katika taarifa ya pamoja kuwa, kuanzia Januari hadi sasa hii ilikuwa ndio duru ya mazungumzo ambayo yamefanyika zaidi katika hali ya mtawalia.

Taarifa hiyo ya Troika ya Ulaya imeendelea kueleza kwamba, "pande zote zinajua kuwa, tunakaribia kufikia hatua ya mwisho ambayo inahitaji maamuzi ya kisiasa; kwa hivyo washiriki wa mazungumzo watarejea miji mikuu yao kwa mashauriano."

Awali, duru moja ilitangaza kuwa, kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa kati ya jumbe za wawakilishi katika mazungumzo ya Vienna, duru ya nane ya mazungumzo itakuwa na wiki moja ya mapumziko.

Na kwa msingi huo, wawakilishi katika mazungumzo, leo watarejea kwenye miji mikuu yao kwa ajili ya mashauriano.

Mapema na kabla ya ufafanuzi uliotolewa na duru hiyo, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Vienna Enrique Mora alieleza katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter kuwa, duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna ambayo ilianza tarehe 27 Desemba, ikiwa ni moja ya duru ndefu zaidi za mazungumzo kuwahi kufanywa hadi sasa, imefikia kwenye kipindi cha mapumziko.

Katika kipindi cha siku za karibuni washiriki katika mazungumzo ya Vienna walikuwa wameshughulika na ukamilishaji wa rasimu ya matini ya makubaliano na uchukuaji maamuzi kuhusu baadhi ya maudhui zilizozusha tofauti.

Katika duru hii ya mazungumzo na kwa mujibu wa makubaliano baina ya pande zote husika, mazungumzo yalifanyika katika ngazi ya kitaalamu na kisiasa kujadili uondoaji vikwazo, kuwepo hakikisho na kupatikana uthibitisho wa Marekani kutekeleza majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../

Tags