Jan 29, 2022 10:56 UTC
  • New York Times: Israel imekuwa ikitumia programu ya kijasusi ya Pegasus kupeleka mbele malengo yake

Gazeti la The New York Times la Marekani limefichua kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umetumia programu ya kijasusi ya "Pegasus" kuendeleza siasa zake za uhasama.

Gazeti la New York Times jana Ijumaa liliripoti kuwa, kampuni ya Israel ya NSO imekuwa ikiuza programu ya kijasusi ya Pegasus kwa mashirika ya kijasusi na vyombo vya sheria vya nchi mbalimbali ikiwemo Marekani kwa takriban muongo mmoja ili kupeleka mbele siasa za kihasama za utawala wa Kizayuni.

Ripoti ya New York Times imeongeza kuwa, kashfa nyingi na ripoti za udukuzi wa simu za idadi kubwa ya waandishi wa habari na wapinzani na tawala mbalimbali duniani mwishoni mwa mwaka jana wa 2021 ziliifanya Wizara ya Biashara ya Marekani iiweke kampuni ya Kizayuni ya NSO katika orodha ya taasisi ambazo harakati na kazi zao zinapingana na usalama wa taifa au maslahi ya sera ya nje ya Marekani.

Hatua hiyo ya serikali ya Marekani iliukasirisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwa sababu kampuni ya Kizayuni ya NSO inaweza kukabiliwa na matatizo makubwa bila ya kupata vifaa vya kielektroniki vya Dell au kutumia sava za  Amazon.

Uchunguzi wa mashirika zaidi ya 17 ya habari inaonesha kuwa, programu ya kijasusi ya Pegasus, iliyotengenezwa na kampuni ya NSO ya Israel, imekuwa ikitumika kujasisi simu za mamia ya waandishi wa habari, wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, pamoja na wanasiasa duniani kote. 

Israel imeuza programu ya kijasusi ya "Pegasus" kwa nchi kadhaa, zikiwemo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Miongoni mwa wanasiasa ambao simu zao zilidukuliwa kwa kutumia programu ya kijasusi ya Pegasus ni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Tags