Jan 29, 2022 12:16 UTC
  • Takwa la Russia kwa ajili  ya kuondoka haraka vikosi vamizi ajinabi huko Syria

Dmitry Polyanskiy Naibu Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema katika hotuba yake katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kuwa Russia inataka kuondoka haraka iwezekanavyo vikosi vyote vamizi ajinabi ambavyo vipo kinyume cha sheria huko Syria.

Dmitry Polyanskiy amesema kuwa ni dhahir shahir kikamilifu kuwa Marekani hata katika uga wa ndani pia haiendeshi vita dhidi ya ugaidi sasa iweje eti itake kukabiliana na suala hilo kimataifa. Polyanskiy ameendelea kubainisha kuwa maeneo ambayo Marekani inahusika moja kwa moja katika kuiba mafuta yameathiriwa na maafa ya mazingira; huku Umoja wa Mataifa pia ukipuuza na kutotilia maanani maafa hayo. Dmitry Polyanskiy Naibu Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa wana wasiwasi mkubwa na mashambulizi hayo ya kibubusa ya kikosi cha anga cha wanajeshi vamizi wa Marekani huko Syria.  

Lori la Marekani lililopakia mafuta ya wizi kutoka Syria

Takwa hilo la Russia kwa ajili ya kuondoka Syria wanajeshi wote vamizi linawahusu moja kwa moja wanajeshi vamizi wa Marekani ambao waliingia Syria miaka kadhaa iliyopita katika kalibu ya eti muungano wa kimataifa wa kupambana na Daesh na kwa kisingizio cha kupambana na kundi hilo la kigaidi nchini humo. Hata hivyo kivitendo wanajeshi vamizi wa Marekani hawatekelezi jukumu lolote huko Syria ghairi ya kuwauwa raia wa kawaida na kuiba mafuta ya nchi hiyo. Katika ripoti yake, Gazeti la New York Times limewanukuu maafisa wa kijeshi na wa zamani wa Marekani na kuashiria kufichuliwa jinai za Marekani katika  mauaji ya raia kupitia mashambulizi ya anga na oparesheni za vikosi maalumu vya nchi hiyo huko Syria. 

Magaidi wa Daesh nchini Syria 

Leonid Slutsky Mkuu wa Kamisheni ya Masuala ya Kimataifa katika Bunge la Russia (Duma) anasema: Wananchi wasio na ulinzi na raia wa kawaida mara kwa mara wamekuwa wakishambuliwa na kudhurika katika oparesheni za vikosi vamizi vya Marekani si tu huko Syria bali hata huko Iraq na Afghanistan pia wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya Marekani.  

Jinai na hujuma za uharibifu wa Marekani huko Syria katika kipindi cha muongo mmoja wa karibuni kimsingi zilikuwa na hatua zilizoratibiwa kwa mpangilio na zenye malengo maalumu. Marekani wakati wa utawala wa Rais Barack Obama kuanzia mwaka 2011 iliyaunga mkono kwa hali na mali makundi ya kigaidi huko Syria lengo likiwa ni kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al Assad na kudhoofisha mhimili wa muqawama. Aidha katika marhala iliyofuata serikali ya Obama yaani mwaka 2014 ilianzisha mashambulizi ya anga na nchi kavu huko Syria sambamba na kutuma wanajeshi huko Syria kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh; nchi ambayo ndiyo iliyoliasisi na ndiyo iliyokuwa ikiliunga mkono pakubwa kundi hilo. Baada ya hapo, Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump aliunga mkono uwepo wa wanajeshi vamizi wa nchi hiyo huko Syria na kisha kuanza kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya nchi hiyo na kuiba mafuta kwa kisingizio cha kupambana na Daesh. Vikosi vamizi vya Marekani vilijikita katika maeneo ya mashariki mwa Syria maeneo ambayo kuna visima na taasisi za gesi na mafuta ya nchi hiyo na kuanza kupora mafuta ya nchi hiyo. Marekani imekuwa ikiyahamisha mafuta ya Syria kupitia ardhi ya Uturuki.  

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama 

Hivi sasa pia serikali ya Biden inapuuza na kukuika misingi na sheria za kimataifa kama haki za mamlaka ya kujitawala nchi na vilevile umoja wa ardhi nzima ya Syria na inaendelea kutekeleza mashambulizi ya anga katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita bila ya kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Rais Joe Biden anaendeleza sera hizo hizo za mtangulizi wake yaani Trump mkabala wa mhimili wa muqawama na Syria. Kuhusu mashambulizi ya anga ya muungano eti ulio dhidi ya  Daesh huko Syria, John Kirby Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ametangaza kuwa hawamuombi yeyote kibali kwa ajili ya kutekeleza mashambulizi hayo tajwa na kusisitiza kuwa,  hawahitajii kibali chochote kwa ajili ya wanajeshi wao kutekeleza mashambulizi huko Syria. Hii ni katika hali ambayo hatua ya Marekani ya kung'ang'ania kusalia wanajeshi wake huko Syria imekabiliwa na radiamali mbalimbali kimataifa. Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Disemba mwaka jana alitangaza kuwa, viongozi wa Marekani wanaendeleza uwepo wa vikosi vyake vamizi kinyume cha sheria huko Syria. Moscow inaamini kuwa, Washington si tu inakwamisha kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia ya kisiasa bali imeyatumia makundi ya kigaidi kama wenzo huku makundi hayo yakichochea vita dhidi ya serikali halali ya Syria. 

Kuwepo kijeshi Marekani huko Syria na oparesheni za kijeshi za vikosi vamizi vya nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya Syria ni kinyume cha sheria za kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa mashambulizi hayo yanakinzana na hati ya Umoja wa Mataifa na kukiuka waziwazi mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Syria kwa kuzingatia upinzani wa mara kwa mara wa serikali halali ya Syria kwa uvamizi huo. 

 

Tags