Jan 30, 2022 02:44 UTC
  • Kinara wa upinzani Venezuela: Niko tayari kufanya mazungumzo na serikali ya Maduro

Kinara wa upinzani nchini Venezuela ametangaza utayari wake wa kuanza tena kkufanya mazungumzo na serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela sambamba na kuashiria hamu yake ya kuanza tena mazungumzo na serikali ya Caracas amedai kwamba, kukataa kuanza tena mazungumzo kutapelekea kuongezeka mashinikizo ya kimataifa dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Wakati kiongozi huyo wa upinzani anadai hayo, Rais Maduro wa Venezuela amesisitiza mara kadhaa kwamba, Marekani ndio inayobeba dhiba ya kusitishwa mazungumzo baina ya serikali ya Caracas na wapinzani.

Mazungumzo baina ya pande mbili yaliyokuwa yakifanyika nchini Mexico kwa usimamizi wa Norway yalisitishwa Agosti 13 mwaka jana (2021).

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela Januari 23 mwaka 2019 alijitangaza kuwa Rais wa Venezuela na Marekani ikamtambua rasmi mara moja baada ya tangazo hilo. Guaido anafanya kila awezalo kupitia Marekani ili kushika hatamu za uongozi nchini Venezuela. Marekani ni miongoni mwa nchi za awali kabisa zilizomuunga mkono Guaido na kuipinga serikali ya Venezuela. 

Katika miaka ya hivi karibuni Marekani imetumia njia ya mbalimbali kama wenzo wa vikwazo vikubwa vya kiuchumi na kisiasa, kuwasaidia wapinzani wa ndani na kuwapatia himaya na misaada ya kifedha na kisiasa hususan Juan Guaido, kiongozi wa upinzani na hata kumtambua kama Rais wa Venezuela ili kuiondoa madarakani serikali halali ya Maduro, lakini imefeli katika njama zake zote hizo.

Tags