Feb 19, 2022 11:24 UTC
  • Trump 'aliiba' nyaraka za siri za serikali alipohama Ikulu ya White House

Idara ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Marekani imetangaza kuwa, nyaraka za taarifa za siri zimepatikana kwenye maboksi 15 ya kumbukumbu za Ikulu ya White yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump huko Mar-a-Lago, jimboni Florida.

Hayo ni kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Idara hiyo ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa kwa Wizara ya Sheria.

Barua hiyo imetolewa kufuatia ripoti kadhaa kwamba Trump amekuwa akihodhi taarifa hasasi, nyeti na hata za siri za serikali tangu wakati wa kipindi chake cha urais na hata baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Sheria ya serikali kuu ya Marekani inapiga marufuku kuzihamishia sehemu isiyoruhusika nyaraka za siri za serikali.

Hayo yanaripotiwa huku wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani wakitaka wapatiwe taarifa za yaliyomo kwenye maboksi yaliyopatikana kwenye nyumba ya Trump ya Mar-a-Lago; hata hivyo idara hiyo ya nyaraka imesema sheria ya taarifa za kumbukumbu hairuhusu kutoa taarifa hizo.

Maafisa wa Idara ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu wakiwa na maboksi yenye nyaraka

Mbunge wa chama cha Democratic Carolyn Maloney, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uangalizi ya Baraza la Wawakilishi amesema, kufichuliwa kwa ripoti hiyo mpya kumezidisha wasiwasi aliokuwa nao kuhusu namna rais huyo wa zamani wa Marekani alivyokuwa heheshimu sheria ya serikali ya uwekaji kumbukumbu za serikali kuu.

Maloney amesisitiza kuwa, atahakikisha anafuatilia ili kubaini kwa undani zaidi jinsi Trump na washauri wake wakuu walivyokiuka Sheria ya Kumbukmbu za Urais; na kutumia matokeo ya uchunguzi huo kwa ajili ya kuleta mageuzi makubwa ya marekebisho ya sheria hiyo ili kuzuia utumizi mwingine mbaya katika siku za usoni.

Gazeti la Washington Post liliwahi kuripoti kuwa, afisa mmoja wa Mamlaka ya Hifadhi ya Nyaraka aliiomba Wizara ya Sheria kuchunguza ufichuzi wa maboksi 15 ya kumbukumbu za White House yaliyopatika kwenye nyumba ya rais huyo wa zamani wa Marekani huko Palm Beach Florida na kuongeza kuwa, alipokuwa White House, Trump alikuwa na mazoea ya kuchana aina zote mbili za nyaraka za kumbukumbu "nyeti na zisizo na umuhimu" .../

 

 

 

Tags