Mar 09, 2022 08:08 UTC
  • Kuongezeka propaganda za kueneza chuki dhidi ya Russia barani Ulaya

Huku mgogoro ukizidi kuwa mkubwa baina ya Russia na nchi za Magharibi hususan kutokana na kupamba moto mapigano nchini Ukraine, mashinikizo yanayotokana na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia nayo yameongezeka.

Uhakika ni kuwa nchi za Magharibi zimeiwekea vikwazo vya kila namna Russia ili kuidhoofisha. Lakini vikwazo hivyo vinaonekana kuleta madhara makubwa zaidi ya kisiasa na kiuchumi duniani na barani Ulaya kwenyewe mbali na madhara yake kwa Russia.

Nchi za Magharibi ikiwemo Marekani na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya zimeamua kuiwekea vikwazo vya kila namna Russia, si vya kisiasa tu, lakini pia vya kiutamaduni na hata vya michezo. 

Mashirika kama Netflix, Disney na Warner Bros. yameiwekea vikwazo Russia. Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) nalo pia limedhihirisha undumilakuwili wake kwa kujiingiza kwenye siasa kwa kupiga marufuku kutumika bendera na wimbo wa taifa wa Russia katika mashandano yoyote ya timu za Russia za mpira wa miguu.

Nchi za Magharibi zinafanya propaganda sana kuhusu vita vya Ukraine na kufumbia macho kikamilifu jinai zinazofanyika nchini Yemen

Kwa mujibu wa tangazo jingine la FIFA, wachezaji wote wa kigeni wanaocheza katika ligi ya Russia wamelazimishwa kuvunja mikataba yao yote na timu za Russia. Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Wavu (Volleyball) nalo limechukua uamuzi wa kuiondoa timu ya Russia katika Ligi ya Mataifa ya Dunia ya 2022 na nafasi yake imepewa timu ya taifa ya Tunisia.

Hatua hizo za nchi za Magharibi zimekilazimisha Chama cha Soka cha Russia kulishitaki Shirikizo la Soka Duniani (FIFA) na Chama cha Soka cha Ulaya (UEFA) kwa mahakama ya CAS.

Hatua hizo kali zimechukuliwa na nchi za Ulaya dhidi ya Russia katika hali ambayo, licha ya nchi hizo kufanya yote hayo, lakini bado zina wahka na woga wa kuiwekea vikwazo Russia katika masuala ya kiuchumi hususan upande wa mafuta, gesi na makaa ya mawe. 

Hii ni kusema kuwa, Jumatatu, tarehe 7 Machi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani alisema kuwa, nchi yake inapinga kikamilifu vikwazo vya kiwango chochote vya gesi, mafuta na makaa ya mawe dhidi ya Russia. Shirika la habari la AFP lilimnukuuu Bi Annalena Baerbock akisema hayo na kuongeza kuwa, wakati nchi fulani inapowekewa vikwazo, inabidi kuweko mikakati madhubuti ya kuendeleza vikwazo hivyo kwa muda mrefu. Lakini kuiwekea vikwazo nchi kwa muda wa wiki tatu na baadae tugundue kuwa hatuwezi kuendelea na vikwazo hivyo, kwa kweli hilo ni jambo lisilo na maana hata kidogo. Alisema, iwapo Ujerumani itapiga marufuku kuingia nchini humo mafuta, gesi na makaa ya mawe kutoka Russia na baada ya kupita siku chache igundulike kuwa umeme umekatika nchini Ujerumani, sisi wenyewe tutalazimika kutia ulimi puani na kuondoa wenyewe vikwazo hivyo. Ujerumani si nchi pekee ya Ulaya inayopinga vikwazo vya kiuchumi na kifedha kwa Russia. Kwa miaka mingi sasa nchi za Ulaya zinajaribu kutokuwa tegemezi kwa nishati ya Russia lakini hadi hivi sasa zimeshindwa. Karibu asilimia 40 ya gesi inayotumiwa na nchi za Ulaya inatokea Russia. 

Annalena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani

 

Pamoja na utegemezi wao huo, lakini kila siku nchi za Ulaya zinaendesha propaganda kubwa ya kuharibu jina la Russia. Kama ambavyo ajenda kuu ya vyombo vya habari vya Magharibi ni kuonesha sura isiyo sahihi kuhusu Uislamu na Waislamu, hivi sasa wimbi la propaganda hizi limeelekezwa dhidi ya Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov amezishutumu na kuzilaumuu vikali nchi za Ulaya na Magharibi kwa propaganda zao hizo na kusema kuwa, hata hatua ya nchi za Ulaya za kutuma magaidi na silaha za hatari nchini Ukraine, zinatokana na wendawazimu wao wa kueneza chuki dhidi ya Russia. Amezitahadharisha nchi za Ulaya kwamba, uwendawazimu wao huo ni hatari kwa usalama wa nchi za Ulaya zenyewe hasa kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana kutokana na siasa hizo za nchi za Magharibi za kuunda magenge ya kigaidi na kuyapa silaha na mafunzo ya kijeshi katika nchi kama za Iraq na Syria, na matokeo yake magaidi hao hao wametumia silaha hizo kufanya mashambulio ndani ya nchi za Ulaya na Marekani. 

Tags