Mar 12, 2022 06:53 UTC
  • WHO inaanza kujadili vipi na lini itangaze kumalizika kwa janga la COVID-19

Wataalamu wa afya ya jamii katika Shirika la Afya Duniani WHO wameanza kujadili vipi na lini itangazwe kumalizika kwa janga la dunia nzima la maradhi ya COVID-19, tukio linalotazamiwa kuwa na umuhimu kihistoria baada ya kupita zaidi ya miaka miwili tangu kilipojitokeza kirusi cha maradhi hayo.

Hata hivyo shirika lenyewe la afya duniani linasisitiza kuwa kwa sasa halifikirii kutoa tangazo hilo. Badala yake, majadiliano yanayoendelea mjini Geneva, yaliko makao makuu ya WHO yanajikita katika kuchunguza mazingira yatakayobainisha hatimaye kwamba hali hatari kiafya iliyotangazwa na shirika hilo Januari 30, 2020 imemalizika.

Ujumbe wa baruapepe uliotolewa na WHO umesema, "Kamati ya Kimataifa ya Taratibu za Dharura za Afya ya Covid-19, inachunguza kigezo kinachohitajika kutumiwa ili kutangaza kuwa hali ya dharura ya afya iliyoibua wasiwasi kimataifa imemalizika".

Hayo yanaripotiwa huku mataifa mengi duniani yakiwa tayari yameshachukua hatua za kurejea kwenye mazingira ya kawaida ya kijamii kwa kulegeza masharti ya uvaaji barakoa, karantini na kufungua mipaka kwa ajili ya safari.

 

Hata hivyo sambamba na hatua hizo, Shirika la Afya Duniani limeripoti kuwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita vimeripotiwa vifo vya watu 52,000 na maambukizi ya watu zaidi ya milioni 10 duniani ya virusi vya corona.

Wakati huohuo, huku kesi za vifo na maambukizi ya corona zikiwa zimepungua katika maeneo mengi duniani, maambukizi yameongezeka ghafla huko Hong Kong, huku China nayo ikitangaza katika juma hili kesi mpya zaidi ya elfu moja kwa siku za maambukizi ya kirusi cha corona cha spishi ya omicron katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kuripotiwa kiwango hicho katika kipindi cha miaka miwili sasa.../

Tags