Mar 12, 2022 07:27 UTC
  • Venezuela: Tutazipatia Ulaya na Marekani mafuta ikiwa vikwazo vitaondolewa

Mwenyekiti wa kamati ya mafuta na nishati katika Bunge la Venezuela amesema, ikiwa vikwazo vitaondolewa, nchi hiyo inaweza kudhaminii mahitaji ya nishati ya Marekani na Ulaya mnamo katikati ya mwaka huu.

Kwa muda wa miongo kadhaa sasa Russia imekuwa ni muuzaji mkubwa wa gesi asilia kwa nchi za Umoja wa Ulaya; na pande hizo mbili zimekuwa zikinufaika katika kudhaminiana mahitaji yao.

Hata hivyo baada ya kuanza vita nchini Ukraine mnamo Februari 24, na kuzuka wasiwasi wa kusitishwa usafirishaji gesi ya Russia kuelekea Ulaya ya Kati, nchi za Ulaya zimeanza kuchukua hatua ya kushauriana na nchi zingine zinazouza bidhaa hiyo.

Angel Luis Rodriguez, mwenyekiti wa kamati ya mafuta na nishati katika bunge la Venezuela amesisitiza kuwa, ili kuweza kufikia mapatano, Marekani inapaswa iipatie Caracas pendekezo la kuvutiia, kwa sababu Marekani ndiye msababishaji mkuu wa kuvurugika kwa hali ya uchumi ya Venezuela.

Angel Luis Rodriguez

 

Mbunge huyo wa Venezuela amesema, ana matumaini kwamba ikiwa nchi hiyo itaanza tena kusafirisha mafuta kuelekea Marekani na Ulaya, hatua hiyo haitaathiri uhusiano wake na Russia.

Wakati huohuo ujumbe wa serikali ya Marekani uko nchini Venezuela kwa mazungumzo kuhusiana na kile kilichotajwa kuwa ni "usalama wa nishati na kulinda uchumi wa Marekani".

Duru zilizo karibu na mazungumzo hayo yaliyoanza mwanzoni mwa juma hili, ambayo yanatajwa kuwa yanatumiwa na Mareanii ili kuitenganisha Venezuela na Russia zimeripoti kuwa, mashauriano hayo hayajapiga hatua ya maana, lakini pande mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo zaidi.

Katika miaka ya karibuni, Washington imetumia vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi, sambamba na kuunga mkono hujuma na hatua haribifu dhidi ya Venezuela, kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Caracas yenye muelekeo ulio dhidi ya Marekani; hata hivyo hatua hizo zimegonga mwamba hadi sasa kutokana na muqawama na kusimama  imara wananchi wa Venezuela.../

Tags