Mar 12, 2022 10:43 UTC
  • Kuwepo kwa wapiganaji wa kigeni katika vita vya Ukraine; mwelekeo na sura mpya

Sambamba na kuendelea vita huko Ukraine, kuwepo kwa vikosi na wapiganaji wa kigeni kumevipa vita hivyo sura na mwelekeo mpya. Ni baada ya Rais Vladimir Putin wa Russia kuafiki suala la kuwezesha wapiganaji na vikosi vya kujitolea vinavyounga mkono nchi hiyo kushiriki katika vita vya Ukraine.

Putin amesema katika mkutano wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia kwamba, mtu yeyote anayetaka kuwasaidia watu wa Donbass, "kwa hiari na sio kwa pesa", anapaswa kuwezeshwa kushirikiana nao na kwenda kwenye maeneo ya vita.

Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu pia alisema katika mkutano huo kwamba idadi kubwa ya watu 16,000 walioomba kwenda kusaidia jamhuri zilizotangaza kujitalawa za mashariki mwa Ukraine wanatoka Asia Magharibi. Vilevile vituo vya jeshi la Russia katika miji mbalimbali ya Syria vinasajili watu wa kujitolea kwa ajili ya kupigana vita nchini Ukraine.

Inaonekana kuwa, hatua hii mpya ya Moscow ya kuwezesha kupelekwa wapiganaji wa kigeni katika vita vya Ukraine, ambao watapigana kwa niaba ya Russia, ni jibu la moja kwa moja kwa hatua ya serikali inayoungwa mkono na nchi za Magharibi ya Ukraine ya kuwahimiza wapiganaji wa kujitolea wa kigeni kujiunga na eti "jeshi la kimataifa la kuitetea Ukraine." Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alitangaza mnamo Februari 27 katika taarifa kwenye tovuti ya rais kwamba nchi yake inaanzisha kitengo cha kimataifa cha wapiganaji wa kujitolea wa kigeni kusaidia katika vita dhidi ya Russia. Baadaye, Rais wa Ukraine alitia saini amri ya kuidhinisha utekelezaji wa haraka wa "mfumo wa muda wa kufuta visa" kwa wageni wanaotaka kutoa msaada wa kuitetea nchi. 

Kyiv inadai kuwa wapiganaji 16,000 wa kigeni wamejiunga au watajiunga na eti "jeshi la kimataifa" katika siku za usoni. Siku tatu zilizopita, kundi la kwanza la wapiganaji wa kujitolea wa kigeni liliwasili nchini Ukraine. Inasemekana kuwa aghlabu ya wanajeshi na wapiganaji hao wa kigeni ni raia wa Marekani, Mexico, India, Sweden na Uingereza. Awali, raia kadhaa wa Georgia waliingia Ukraine kupigana dhidi ya Russia, akiwemo waziri wa zamani wa ulinzi wa Georgia. Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vimekuwa na nafasi kubwa katika kujenga hali ya kisaikolojia katika mchakato huu, yaani, kuhimiza raia wa nchi kigeni kujiunga na eti jeshi la kimataifa la kutetea Ukraine. Wanajeshi na wapiganaji hao wa kigeni wanaopelekwa Ukraine kupigana na Russia wanalipwa kitita kikubwa cha fedha. 

Daesh

Wamagharibi na washirika wao pia wana nafasi kubwa katika uwanja huu. Idara ya Ujasusi wa Nje ya Russia (SVR) ilisema katika taarifa yake ya tarehe nne mwezi huu wa Machi kwamba Marekani inawapa mafunzo magaidi wa Daesh (ISIS) katika kambi ya kijeshi ya cha Al-Tanf nchini Syria ili wapelekwe kupigana Ukraine. Taarifa ya SVR imeongeza: “Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Kamandi ya Operesheni Maalumu ya Marekani inaendelea kuunda vitengo vipya vya Daesh Magharibi mwa Asia na nchi za Afrika na imepangwa kuwa, magaidi hao watapelekwa Ukraine kwa kushirikiana na mashirika ya ujasusi ya nchi wanachama wa shirika la NATO. Marekani imepanga kuwatumia magaidi hao wa Daesh katika kazi za uharibifu na hujuma za kigaidi dhidi ya Russia nchini Ukraine kupitia ardhi ya Poland.”

Inatupasa kusema hapa kuwa, Marekani haiko peke yake katika suala hili, kwani Uturuki, mwanachama mwingine wa NATO ambaye amepata uzoefu sawa na kutuma magaidi wa kitakfiri huko Libya na Nagorno-Karabakh, pia inashiriki katika kutuma magaidi huko Ukraine. Mwaka 2020 Uturuki ilituma takriban magaidi 1,000 kutoka Syria hadi Nagorno-Karabakh kushiriki katika vita dhidi ya Armenia na walibaki huko baada ya kumalizika kwa vita, na sasa wamepelekwa Ukraine kushiriki katika vita dhidi ya Russia. Saeed Faris al-Saeed, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kistratijia amesema: "Magaidi 2,500 waliopo katika mkoa wa Idlib huko Syria wako tayari kushiriki katika vita dhidi ya Russia. Idara ya Ujasusi ya Uturuki inasimamia kazi ya kuwahamisha magaidi hao hadi Poland na kisha Ukraine, na wengi kati ya magaidi hao wana uraia wa Syria, nchi nyingine za Kiarabu au Chechnya.” Karibu magaidi wa kigeni wapatao 450 wenye mafungamano na makundi yanayojulikana kwa jina la "Al-Turkestani", "Hurrasuddin" na "Ansar Al-Tawhid" wamepelekwa Ukraine kupitia mpaka wa Uturuki.

Sasa, katika kujibu hatua ya nchi za Magharibi na washirika wao ya kutuma vikosi na wapiganaji wa kujitolea wa makundi ya kigaidi na kitakfiri kushiriki katika vita vya Ukraine, Putin ametoa amri ya kuwezesha wapiganaji 16,000 wa kujitolea wa kigeni kwenda kuwasaidia watu wa Donbass.

Kwa utaratibu huu inaonekana kuwa, vita vya Ukraine vinabadilika taratibu kutoka hali ya vita kati ya nchi mbili na kupata mwelekeo na sura ya kimataifa.

Tags