Mar 14, 2022 02:53 UTC
  • Kukiri EU kosa lake la kuiahidi Ukraine kujiunga na NATO

Josep Borrell Fontelles, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amekiri kuwa kitendo cha umoja huo cha kuipa ahadi Ukraine ya kuiunga na Jeshi la Nchi za Magharibi NATO, lilikuwa kosa.

Borrell amesema, sisi tulitoa ahadi ambazo hatukuweza kuzitekeleza hususan kuhusu kujiunga Ukraine na NATO. Ahadi hiyo hatukuitekeleza kabisa. Nafikiri kuwa hilo lilikuwa kosa, kwamba tulitoa ahadi na hatukutekeleza.

Mkuu huyo wa masuala ya kidiplomasia ya Umoja wa Ulaya amekiri pia kwamba Magharibi imefanya makosa katika uhusiano wake na Russia kwani badala ya nchi hizo za Magharibi kuiweka Russia karibu yao, zimezidi kuisukuma mbali na kujenga uadui nayo.

Matamshi hayo ya Borrell ya kukiri makosa ya Umoja wa Ulaya hususan katika kadhia ya Ukraine ni aina fulani ya kukiri kuwa Magharibi ndiyo yenye makosa katika kuzuka mgogoro mashariki mwa Ulaya na hatimaye kutokea vita nchini Ukraine. Mwaka 2008, viongozi wa Jeshi la Nchi za Magharibi NATO walikutana mjini Bucharest, Romania na kutangaza uamuzi wao wa kuziingiza katika NATO nchi mbili za Ukraine na Georgia ambazo ziko kwenye eneo la ushawishi wa Russia, ikiwa ni katika muendelezo wa hatua za kichokozi za nchi za Magharibi za kuibana zaidi na zaidi Russia katika mipaka yake. Tangu mwaka huo jambo hilo na hususan suala la uanachama wa Ukraine katika NATO limekuwa ni jambo lenye mgogoro baina ya Russia na nchi za Magharibi.

Josep Borrell Fontelles, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya

 

Kichekesho hapa ni kwamba, Ukraine imekumbwa na vita vya pande zote na Russia, lakini nchi za Ulaya na Marekani zimekataa kujiingiza vitani kuisaidia Ukraine katika vita vyake hivyo ambavyo vimechochewa na hao hao Wamagharibi. Josep Borrell alidai siku ya Jumamosi kwamba, Umoja wa Ulaya umeamua kutoingia kwenye vita nchini Ukraine kwani unataka kuepusha kutokea vita vikubwa na vya pande zote vya dunia.

Msimamo huo umelalamikiwa vikali na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, ambaye ametoa maneno makali kiasi kwamba amesema, hivi hizo nchi za Magharibi zina uwezo wa hata kulinda wananchi wao? Alisema kuwa, damu zote zinazomwagika katika vita vya Ukraine, lawama zake zinakwenda kwa nchi hizo za Magharibi. Matamshi hayo ya Zelenskyy ni uthibitisho kwamba sasa ameelewa kosa lake la kusikiliza ahadi chapwa za nchi za Magharibi ambazo zilionesha huko nyuma kuwa zitakuwa pamoja na Ukraine kwa hali yoyote ile kama itafanya uadui na Russia. James Tweedie, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa habari wa Marekani anasema, Marekani imeichochea Ukraine kujitumbukiza kwenye vita na Russia na Ukraine nayo ikaandaa mazingira ya kushambuliwa na Russia.

Ukraine ilivyochakazwa na vita

 

Tab'an nchi za Magharibi hivi sasa zimeiwekea Russia vikwazo vikali sana kwa kisingizio cha vita vya Ukraine na zinatuma misaada mikubwa ya kijeshi, kisilaha na taarifa za kijasusi kwa Ukraine. Pamoja na hayo, wanachama wote wa NATO, iwe nchi za Ulaya au Marekani, zimekataa katakata  kujiingiza kwenye vita vya moja kwa moja na Russia huko Ukraine. Zimekataa hata kutangaza eneo lililo marufuku kupaa ndege zikihofia kuingia kwenye vita vya moja kwa moja na Russia. Rais wa Ukraine alizing'ang'ania sana nchi wanachama wa NATO zitangaze eneo lililo marufuku kupaa ndege nchini humo lakini hilo lilikuwa na maana kwamba, nchi hizo zingeliitungua ndege yoyote ya Russia inayoshiriki kwenye vita vya Ukraine itakayopita kwenye eneo hilo; suala ambalo ni la hatari mno. Russia ilitangaza mapema kuwa, nchi yoyote itakayotumia eneo lake kushiriki kijeshi kwenye vita vya Ukraine itahesabiwa na Moscow kuwa ni uwanja wa mapigano ambao unapaswa kushambuliwa na Russia. Kwa hatua yao ya kumkatalia Zelenskyy ombi lake la kutangaza eneo lililo marufuku kupaa ndege nchini Ukraine, wanachama wa NATO, iwe ni Marekani au nchi za Ulaya, zilituma ujumbe usio wa moja kwa moja kwa Ukraine kwamba, isitegemee kuwa NATO itaingia vitani, bali Kyiv inapaswa kukabiliana peke yake na Russia.

Tags