Mar 14, 2022 02:57 UTC
  • Associated Press: Marekani inatumia dola milioni mbili kwa mwezi kuwalinda wapangaji wa mauaji ya Qassem Soleimani

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, dola milioni 2 hutumika kwa mwezi kutoka kwenye mifuko ya walipakodi nchini Marekani kuwalinda wanasiasa wawili wa Republican wenye msimamo mkali wa utawala wa Donald Trump na wahusika wa mauaji ya Kamanda Qassem Soleimani.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema inatumia dola milioni 2 kwa mwezi kulipia ulinzi wa kila siku wa waziri wa zamani wa mambo ya nje, Mike Pompeo na Brian Hook, aliyekuwa mjumbe maalumu wa serikali ya Donald Trump katika masuala ya Iran.

Ripoti ya wizara hiyo kwa Kongresi ya Marekani imesema kwamba gharama za kumlinda Pompeo na Brian Hook kufikia Februari mwaka huu 2022 ilikuwa dola milioni 13.1.

Pompeo na Hook waliongoza kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi ya utawala wa Trump dhidi ya Iran, na ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema kwamba, kwa mujibu wa tathmini za kijasusi, vitisho dhidi ya watu hao wawili vinaendelea hata baada ya kuondoka madarakani utawala wa Trump.

Hapo awali, televisheni ya CBS News iliripoti kwamba utawala wa Joe Biden ulikuwa umepanga hatua za usalama za saa 24 kwa ajili ya kumlinda Brian Hook na Mike Pompeo, maafisa wa zamani wa utawala wa Donald Trump na wapangaji wa mauaji ya Kamanda Qassem Soleimani.

Jenerali Qassem Soleimani

Kabla ya hapo gazeti la The Guardian la Uingereza iliandika kuwa: Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, alikuwa akimhimiza Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump kufanya mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani miezi kadhaa kabla ya kuuawa kwa kamanda huyo akiwa safarini nchii Iraq. 

Pompeo alihalalisha mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani kwa kisingizio kwamba alikuwa tishio la kwa maslahi ya Marekani.

Hata hivyo Inspekta Jenerali wa Umoja wa Mataifa, Agnes Calamard ameitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa akisema hakuna ushahidi wa aina yoyote wa kuunga mkono madai ya Pompeo.

Agnes Calamard

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambaye aliwasili Iraq mnamo Januari 3, 2020 kwa mwaliko rasmi wa maafisa wa Iraqi, aliuawa shahidi katika mashambulizi ya anga na magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq akiwa pamoja na Abu Mahdi al-Mohandes, Naibu Mkuu wa harakati ya Watu wa Iraq  ya al Hashdu al-Shabi na wasaidizi wao 8.

Tags